Samatta aweka rekodi tatu usiku wa Ligi ya Mabingwa

Wednesday September 18 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam.Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta anayeichezea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, ameweka rekodi tatu usiku wa jana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
KRC Genk ikiwa ugenini Austria, ilikubali kipigo cha mabao 6-2 kutoka kwa wenyeji wao, Salzburg huku yakishuhudiwa mabao matatu ya kwanza 'hat trick' ikifungwa na mtoto (Erling Braut) wa mchezaji wa  zamani wa Manchester City, Alf-Inge Håland.
Samatta alianza katika kikosi cha kwanza cha KRC Genk, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kucheza mashindano hayo makubwa.
Samagoal aliweka rekodi nyingine dakika ya 52 ya mchezo huo baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Theo Bongonda kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa  Kitanzania kufunga bao kwenye Ligi hiyo.
Pia bao hilo, lilimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kufunga bao lake la kwanza katika mchezo wa kwanza kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa.
Rekodi nyingine ni Samatta ni kuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kuadhibiwa katika mashindano hayo kwa kadi ya njano baada ya kumchezea vibaya Zlatko Junuzović.
Aliyezamisha jahazi la Genk, alikuwa ni mtoto wa Alf-Inge, Erling, 19, ambaye aliwafunga mabao matatu, ambayo yamemfanya kuingia kwenye rekodi ya kuwa kinda wa tatu Kihistoria kufunga mabao matatu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabao mengine ya Salzburg kwenye mchezo huo, yalifungwa na Hee-Chan Hwang, Dominik Szoboszlai, Andreas Ulmer huku lingine kwa Genk likifungwa na Jhon Lucumi.
Mchezo mwingine wa Kund E ambalo KRC Genk wapo, uliwashuhudia mabingwa watetezi wa Ligi hiyo ya Mabingwa Ulaya, Liverpool wakiwa Italia wakikubali kipigo cha mabao 2-0, yaliyozamishwa na Dries Mertens kwa mkwaju wa penati na Fernando Llorente.
Oktoba 2, KRC Genk watakuwa nyumbani kuwakaribisha wababe wa Liverpool, Napoli huku shughuli nyingine kwenye kundi hilo, ikiwa kati ya majogoo wa jiji ambao wameanza watakuwa Anfiled, kucheza na Salzburg.

Advertisement