UCHAMBUZI: Ni aibu wakazi Mara kushindwa kuwajali walimu

Beldina Nyakeke

Novemba 14 majira ya saa 2 asubuhi Mwalimu Justine Ogo (30) ambaye alikuwa ni mwalimu wa kujitolea akifundisha masomo ya Historia na Kingereza katika Shule ya Sekondari ya Itiryo katika halmashauri ya wilaya ya Tarime vijijini, aliuawa kwa kuchomwa na mkuki.

Mwalimu huyo aliuawa akiwa katika harakati za kulitumikia Taifa ambapo alikuwa akiwahi kwenye usimamizi wa mitihani ya Taifa ya kidato cha pili akiwa amewapakia walimu wenzake wawili kwenye pikipiki.

Tukio la kuuawa kwa mwalimu huyo kijana linahusishwa na mila na tamaduni potofu ambapo inadaiwa kuwa liliratibiwa na baadhi ya wazee wa mila, ili kuweza kufanikisha zoezi la tohara ambalo lilifanyika kuanzia Novemba 15 kwa koo ya Wairegi kutoka katika kabila la Wakurya.

Tukio hilo lisilo la kawaida japo kwa baadhi ya koo za kabila la Kikurya ni suala la kawaida kimila, liliamsha hisia kali kwa baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mara ambao si Wakurya na zaidi watumishi wa umma wa kada mbalimbali hasa walimu.

Nasema hasa walimu kwa sababu mwenzao ndio aliyekuwa mwathirika wa tukio hilo la mauaji yanayohusishwa na kafara ya damu, ili kufanikisha tohara achilia mbali watumishi na raia wengine wasiyo Wakurya. Ilivyo ni kuwa hadi sasa walimu zaidi ya kumi wa shule hiyo wametishia kuacha kazi iwapo hawatohakikishiwa usalama wao.

Tukio la mwalimu huyu kuuawa ni moja tu ya mifano jinsi ambavyo walimu mkoani Mara wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo mila, tamaduni na desturi potofu zinazoendekezwa na baadhi ya koo ama makabila ya mkoa huu.

Yamekuwepo matukio kadhaa yanayowakumba walimu na watumishi wengine wa umma katika vituo vyao vya kazi hapa mkoani Mara, ikiwamo yale yanayohusishwa na imani za kishirikina, kuvamiwa na kukatwa mapanga, kutishwa wakati wakitekeleza majukumu yao na viongozi wa kisiasa kutumia mamlaka yao vibaya.

Mwaka jana mwanzoni kulizuka vitendo vya kishirikina katika baadhi ya shule katika halmashauri ya wilaya ya Musoma Vijijini, ambapo baadhi ya walimu ambao si wazawa wa wilaya hiyo walikumbana na kadhia mbalimbali ikiwamo kujikuta wamelala nje ya nyumba, wengine kunyolewa sehemu za siri, chakula/mboga kuliwa na watu wasiojulikana nyakati za usiku.

Hali hiyo ilisababisha viongozi wa halmashauri kutishia kuwahamisha walimu wote katika shule hizo kutokana na vitendo hivyo kukithiri.

Hayo na mengine mengi ambayo sikuyataja hapa ni baadhi tu ya madhila yanayowakumba watumishi hao wa umma na kusababisha morali ya ufundishaji kushuka na hatimaye baadhi yao pengine kufikia hatua ya kuona hakuna haja tena ya kuendelea na kazi.

Cha kushangaza mkoa unapofanya vibaya kitaaluma wakazi wa mkoa huu hukimbilia kuwanyooshea vidole viongozi wa umma wakidai kuwa wameshindwa kusimamia suala la elimu. Sasa watasimamia vipi wakati walimu kama nyenzo muhimu hawatendewi haki wala kupewa hadhi stahili?

Hivi sasa kwa mujibu wa ofisi ya elimu ya mkoa, karibu walimu wote wa mkoa wa Mara wanaomba kuhamishwa, kutokana na mazingira magumu ya kazi ambayo yanasababishwa na jamii yenyewe.

Ikumbukwe kuwa walimu hawa wapo mkoani Mara kwa ajili ya kuwafundisha watoto wa wenyeji wa mkoa huo, lakini wahusika hawataki kuwatengenezea walimu mazingira rafiki.

Walimu hawa hawa bado wanalalamikia masuala mbalimbali ya maslahi yao kama vile mishahara kidogo, malimbikizo ya madeni wanayodai kama vile likizo, uhamisho na madai mengineyo.

Katika hali kama hiyo nilitegmea jamii ya watu wa Mara ingekuwa mstari wa mbele kuwasogeza na kuwakumbatia walimu ili angalau wawaondolee machungu na magumu ya kiutumishi waliyo nayo. Lakini cha ajabu jamii nayo imegeuka kuwa adui. Walimu wakimbilie wapi?

Umefika wakati sasa watu wa Mara waone umuhimu wa elimu na pia waweze kubadilika na kuwachukulia walimu kama marafiki na kuwa nao karibu muda wote ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Beldina Nyakeke ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Mara. 0784 561 531