UCHAMBUZI: Takwimu zitusaidie ujenzi wa vyumba vya madarasa

Tuesday January 28 2020

 

By Beldina Nyakeke

Kila kona nchini ni habari za uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza pamoja na wale wa sekondari bila kuwasahau wale wa awali.

Pamoja na pilikapilika hizo lakini jambo kubwa ambalo linaumiza vichwa vya watu wengi wakiwamo viongozi wa Serikali, wazazi pamoja na wadau wa elimu, ni suala la upungufu au ukosefu wa vyumba vya madarasa na madawati katika shule nyingi za umma.

Zaidi ya nusu ya mikoa nchini imeripotiwa kuwa na tatizo la upungufu wa madarasa, hali iliyosababisha viongozi wa Serikali kuingilia kati na kuagiza viongozi wa mikoa, wilaya na mamlaka nyingine kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu wanaanza masomo kwa pamoja jambo ambalo ni jema sana.

Nasema kuwa jambo hili ni jema kwa vile limesaidia watoto wote kuanza masomo kwa pamoja tofauti na kipindi cha nyuma ambapo kuna baadhi ya meneo wanafunzi walichelewa kuanza masomo kwa sababu ya awamu za uchaguzi wa wanafunzi.

Kulikuwepo na chaguo la kwanza, kisha chaguo la pili pamoja na mengine ambayo yalikuwa yakifanyika kulingana na upatikanaji wa nafasi katika shule za umma.

Kuwapo kwa awamu tofauti za uchaguzi kwa namna moja ama nyingine kulikuwa kunawaumiza wanafunzi wanaochaguliwa baadaye kutokana na ukweli kwamba walikuwa wanatakiwa kufanyakazi zaidi ili waweze kuwafikia wenzao walioanza mapema.

Advertisement

Umefika muda sasa mamlaka husika ziangalie namna ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hii ya upungufu wa madarasa na madawati ili watoto waweze kusoma kwa amani sambamba na walimu kuweza kupata muda wa kutosha kutimiza wajibu wao.

Changamoto hii sasa imekuwa ikijirudia kila mwaka kiasi kwamba inakuwa ni sehemu ya maisha yetu wakati upo uwezekano wa kuitatua mapema kabisa na watoto wetu wakaweza kujiunga na kuanza masomo kwa wakati.

Changamoto hii inaweza kutatuliwa kwa kufanya maandalizi ya mapema kuliko kusubiri kufanya mambo kwa zima moto, hasa ikijulikana kuwa kila mwaka lazima kuwe na wanafunzi wapya wanaopaswa kuandikishwa shuleni.

Hapa ndipo matumizi ya takwimu yanapofanya kazi kwa vile naamini kuwa Serikali inazo takwimu za wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi sambamba na matokeo ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka unaofuata.

Hivyo basi kwa takwimu hizo ni dhahiri kuwa inajulikana ni vyumba vingapi vya madarasa vitakavyohitajika kwa ajili ya kuwachukua wanafunzi watarajiwa.

Kutokana na takwimu hizo upo uwezekano wa kupanga namna ambavyo madarasa hayo yanaweza kupatikana na hata kujengwa kwa uimara tofauti na sasa ambapo shaka kuu ni namna madarasa hayo yanavyojengwa pasipo kuzingatia ubora.

Badala ya kuanza kufanya kazi kwa zima moto huku tukiathiri upande mwingine, takwimu hizi zitumike kupanga na kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo kwa vile uwezo wa kujenga upo na ndio maana tumekuwa tukijenga kwa kukimbizana bila sababu za msingi.

Takwimu zikitumika vema na mipango ikawekwa, tatizo la madarasa litakuwa historia kabisa kuliko ambavyo imekuwa sasa desturi yetu kuwa kila ifikapo Januari ni kama mambo yote husimama na sote tunaimba wimbo mmoja wa vyumba vya madarasa na madawati.

Ni aibu kusimamisha mambo mengine kuendelea kwa sababu tu ya ujenzi wa madarasa. Eti kila mwaka hatujui kama kuna wanafunzi wapya wanaotakiwa kujiunga shuleni.

Mipango ikiwekwa kwa muda wa mwaka mzima kwa kuangalia takwimu na matokeo ya wanafunzi watarajiwa kwa mwaka unaofuata, mahitaji ya madarasa na madawati yanaweza kutatuliwa katika kipindi cha mwaka mzima.

Januari ikifika unabakia wajibu wa wazazi kuwapeleka watoto wao shule na si tena muda wa kufukuzana na matofali kujenga vyumba vya madarasa.

Kwa muda sasa naona kisingizio kimekuwa ni ongezeko la wanafunzi shuleni kutokana na utekelezaji wa mpango wa elimu bure.

Sababu hii haina mashiko kwa vile takwimu zipo hivyo tunajua kabisa kuwa mwaka unaofuata wanafunzi wa kidato cha kwanza watakuwa wangapi na mahitaji yao ni kiasi gani hivyo maandalizi yanapaswa kufanyika tangu mapema.

Beldina Nyakeke ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Mara. 0784561531