Abdul Nondo akamatwa kwa ‘kutia’ mguu UDSM

Mwenyekiti wa Mtandao wa wanafunzi (TSN) na Mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo
Muktasari:
Wakili wake asema ni baada ya kuonekana maeneo ya chuo hicho jana.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Mtandao wa wanafunzi (TSN) na Mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo amekamatwa na jeshi la polisi kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuonekana katika maeneo ya chuo hicho.
Akizungumza kwa njia ya simu leo Julai 27, 2018 wakili wa mwanafunzi huyo Jebra Kambole amesema Nondo alikamatwa Julai 26 saa tatu usiku wakati akizungumza na wenzake, katika eneo la chuo hicho.
Inaelezwa kuwa Nondo alikwenda kuchukua vitu vyake chuoni hapo.
Kambole amesema wakati Nondo anaondoka chuoni hapo aliacha baadhi ya vitu ambavyo alilazimika kuvifuata baada ya wenzake kufunga chuo.
“Alikutana na wenzake chuoni hapo wakawa wanajadiliana baadhi ya mambo ndipo askari wa eneo la chuo walimkamata na kumuweka ndani,” amesema Kambole na kuongeza:
“Lakini eneo alilokamwatwa ni ambalo mtu yeyote anaweza kupita kwa sababu hata magari ya kwenda Mwenge yanapita.”
Amesema kwa mujibu wa maelezo ya awali aliyopewa ni kuwa Nondo amekamatwa kwa kosa la kuingia eneo la chuo kinyume cha sheria.
“Lakini katika barua ya kusimamishwa chuo aliyopewa hakuna sehemu iliyoandikwa kuwa hatakiwi kufika eneo la chuo sasa kwanini akamatwe,” amesema Kambole.
Amesema tayari wameshaandaa wadhamini na wanasubiri tu maelezo.