Halmashauri yawatimua watumishi watano kwa ubadhilifu

Muktasari:

Pia, wengine wanadaiwa kuisababishia hasara halmashauri hiyo zaidi ya Sh460 milioni kwa kutokuzingatia taratibu za ununuzi. Kufukuzwa kazi kwa watumishi hao kumefuatatia uamuzi uliotolewa na baraza la madiwani baada ya uchunguzi kukamilika tangu wasimamishwe kazi Mei mwaka huu, hivyo kubainisha kuwa walifanya ubadhirifu wa  fedha za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na zingine za chanjo ya watoto zaidi ya Sh68 milioni.

Nzega. Watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, wamefukuzwa kazi na wengine wawili wameshushwa vyeo kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh190 milioni.

Pia, wengine wanadaiwa kuisababishia hasara halmashauri hiyo zaidi ya Sh460 milioni kwa kutokuzingatia taratibu za ununuzi. Kufukuzwa kazi kwa watumishi hao kumefuatatia uamuzi uliotolewa na baraza la madiwani baada ya uchunguzi kukamilika tangu wasimamishwe kazi Mei mwaka huu, hivyo kubainisha kuwa walifanya ubadhirifu wa  fedha za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na zingine za chanjo ya watoto zaidi ya Sh68 milioni.

Akizungumza katika kikao cha madiwani  Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Marco Kiwele  alisema baada ya uchunguzi menejimenti ya halmashauri, madiwani wamejiridhisha na tuhuma hizo hivyo kwa kuzingatia kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 namba 42 watuhumiwa wamepatikana na hatia.

Amewataja waliofukuzwa kuwa ni aliyekuwa Ofisa Ununuzi, Seleman Cherehani; Mweka Hazina, Stanslaus Kalokola; Katibu wa Hospitali ya Wilaya, Kisasu Sikalwanda; Mratibu wa Chanjo Wilaya, Joel Jondele na Mtendaji wa Kijiji cha Mwamala, Said Madua aambaye anatuhumiwa kutafuna Sh12 milioni.

Walioshushwa vyeo ni aliyekuwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dk Emmanuel Mihayo na aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya, Denis Gombeye. Hata hivyo, jitihada za kuwapata watuhumiwa hao zilishindikana kutokana na kuondoka wilayani tangu waliposimamishwa kazi na kudaiwa kubadilisha namba zao za simu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Jacob James aliwataka watumishi kuwa waadilifu na kuongeza kuwa, ataendelea kusimamia sheria.