Hivi ndivyo hakimu ‘alivyoyeyusha’ hoja za Jamhuri akimuachia Nondo

Muktasari:
Jana Jumatatu Novemba 5, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imemwachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo baada ya kushindwa kumtia hatiani
Iringa/Dar. Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, imemuachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo kutokana na Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka mawili yaliyosababisha afikishwe mahakamani hapo.
Nondo alifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo Machi 21, akikabiliwa na makosa mawili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo kwamba “nipo hatarini” na kuzisambaza mtandaoni.
Kosa la pili, lilikuwa ni kutoa taarifa za uongo kwa askari Polisi, Koplo Salim wa Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa kiwanda cha Pareto mjini Mafinga.
Jana Novemba 5, hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Liad Chamshana akitoa hukumu hiyo alisema katika kosa la kwanza, upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha uongo wa maneno ya mshtakiwa, maana ya maneno ‘nipo hatarini’ na nani aliyesambaza maneno hayo.
Hakimu Chamshana alisema shahidi wa kwanza hadi wa sita hawakuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya kosa hilo na badala yake walitumia hisia na mashaka, jambo lililowafanya washindwe kuithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka kwamba mshtakiwa ndiye aliyeandika maneno hayo ya uongo.
Kwa msingi huo, Chamshana alisema Mahakama imeyaangalia maneno hayo ‘nipo hatarini’ na kujiridhisha kwamba yana maana pana ambayo ni ngumu kuitumia kumuadhibu mshtakiwa huyo.
Alisema upande wa Jamhuri umeshindwa pia kuthibitisha kama Nondo ndiye aliyesambaza maneno hayo, kwa sababu ushahidi wao unaonyesha yalisambazwa na shahidi wao wa tatu ambaye ni mwanafunzi anayesoma pamoja na mshtakiwa huyo UDSM.
Katika kosa la pili, Chamshana alisema upande wa Jamhuri ulishindwa pia kuthibitisha kosa la mshtakiwa huyo aliyekwenda katika Kituo cha Polisi cha Mafinga kama mlalamikaji kabla malalamiko yake hayajageuzwa na kuwa mashtaka yake.
“Upande wa Jamhuri na utetezi wote wanakubali kwamba Machi 7, 2018 mshtakiwa alikuwa Mafinga na alikwenda kituo cha Polisi kutoa malalamiko yake,” alisema.
Alisema cha kushangaza, mashahidi wote saba wa upande wa Jamhuri walishindwa kutoa ushahidi unaoonyesha namna mshtakiwa huyo alivyofika Mafinga na ule unaoonyesha kabla ya kufika Mafinga alikuwa wapi ili kuthibitisha kama alitekwa au alijiteka.
Hakimu Chamshana alishangaa kwa nini vyombo vilivyofanya upelelezi (polisi) dhidi yake viliacha majukumu yao ya kipolisi ili viweze kuthibitisha madai hayo na badala yake vikamchukulia mshtakiwa huyo kama mhalifu.
“Kwa msingi huo Mahakama imeshindwa kuyaamini mashtaka yaliyotolewa na upande wa Jamhuri na hivyo inamuachia huru mwanafunzi huyu,” alisema na kuongeza kwamba upande wa mashtaka unaweza kukata rufaa.