Jela miaka 22 kwa ujangili
Same. Mkazi wa Kiteto mkoani Manyara, Issa Salum (43) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 22 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya ujangili katika Hifadhi ya Mkomazi.
Hukumu hiyo imesomwa leo na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Same, Judith Kamala mbele ya wakili mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme aliyeiendesha kesi hiyo kuanzia Julai mwaka jana.
Katika hukumu hiyo, mahakama imeamuru kutaifishwa kwa bunduki mbili aina ya Rifle pamoja na vipande vinne vya meno ya Tembo vyenye thamani ya Dola 20,000 sawa na Sh40 milioni za Tanzania.
Mshitakiwa huyo aliwahi kutiwa hatiani katika kesi namba 203/2014 ya kuingia katika hifadhi bila kibali na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh350,000 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Babati.