Kifungo cha marais wastaafu chawaibua wasomi, wanasiasa

Muktasari:

Marais wastaafu wa nchi tatu tofauti wamewajibishwa kwa makosa waliyoyafanya wakiwa madarakani wiki iliyopita jambo ambalo limeibua maoni mbalimbali.

Dar es Salaam. Kuwajibishwa kwa marais watatu wiki iliyopita, kumewafanya wasomi na wanasiasa nchini kuwa na maoni tofauti.

Marais wastaafu wa nchi tatu tofauti wamewajibishwa kwa makosa waliyoyafanya wakiwa madarakani wiki iliyopita jambo ambalo limeibua maoni mbalimbali.

Ukiacha Ufaransa, dunia ilishuhudia marais wa Korea Kusini, Brazil na Afrika Kusini wakihukumiwa au kufikishwa mahakamani.

Wakati mahakama za Korea Kusini na Brazil zikiwatia hatiani wastaafu hao, Afrika Kusini iliahirisha kesi hadi Juni mwaka huu.

Baadhi ya waliofuatilia kesi hizo walieleza hisia zao kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, wakisema ni wakati sasa kwa viongozi waliokasimiwa mamlaka kujitafakari na kuacha kudhani kwamba ni kazi kubadilisha dhana ya utawala wa sheria kutoka maneno kwenda kwenye vitendo.

Kushtakiwa na kuhukumiwa kwa marais wastaafu wa Brazil, Korea Kusini na Afrika Kusini kumefanyika wiki iliyopita, siku chache baada ya Rais mstaafu wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy kushtakiwa kwa makosa ya ufisadi na matumizi mbaya ya ofisi ya umma.

Kesi mpya inayomkabili Sarkozy imejikita katika jitihada zake za kutaka jaji amvujishie taarifa kuhusu uchunguzi unaomhusu katika shauri jingine la utumiaji haramu wa fedha kugharimia kampeni zake mwaka 2007.

Nchini Brazil, jaji aliamuru rais mstaafu wa taifa hilo, Luiz Inácio Lula da Silva kujisalimisha kituo cha polisi ili kuanza kutumikia kifungo cha miaka 12 jela kwa makosa yanayohusu ufisadi.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi la Lula la kuitaka mahakama iamuru awe huru wakati akiendelea na rufaa.

Mashtaka ya Lula yanatokana na uchunguzi dhidi ya vitendo vya ufisadi katika ‘operesheni osha gari’ inayowahusu wanasiasa kadhaa wa ngazi za juu kutoka vyama tofauti nchini humo.

Wakati hayo yakijiri katika taifa hilo kubwa la Latini Amerika, nchini Afrika Kusini, rais aliyejiuzulu hivi karibuni, Jacob Zuma ameshtakiwa kwa makosa ya ufisadi yanayohusu ununuzi wa silaha tangu miaka ya 1990.

Zuma anakabiliwa na makosa 16 ya ufisadi, udanganyifu na utakatishaji wa fedha haramu.

Nchini Korea Kusini, rais mstaafu Park Geun-hye amehukumiwa kifungo cha miaka 24 jela baada ya kupatikana na hatia ya utumiaji mbaya wa madaraka na matumizi ya nguvu.

Park, ambaye ametakiwa kulipa faini ya dola 17 milioni za Marekani (takriban Sh37.91 bilioni), anakabiliwa na mlolongo wa kesi za ufisadi.

Hata hivyo, marais wote wanne wamekana kuhusika na makosa yanayowakabili, wakidai ni ya kisiasa.

Ni tahadhari

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda anayaona matukio hayo kama tahadhari kwa walio katika nafasi za uongozi wa umma.

Anaamini wengi kati ya waliokasimiwa madaraka husahau kwamba vyeo walivyonavyo ni dhamana waliyopewa na wananchi.

Dk Mbunda alisema wanapaswa wazingatie misingi ya kidemokrasia wakati wa kutekeleza shughuli zao za kila siku.

“Wanadhani hawagusiki,” alisema Dk Mbunda alipozungumza na The Citizen, gazeti dada la Mwananchi.

Alisema baadhi ya viongozi madaraka huwalevya hivyo kutumia vibaya ofisi za umma kufanya upendeleo na matendo mengine yasiyofaa.

Mwanasheria mkongwe, Profesa Abdallah Safari alisema rais anaweza kushtakiwa baada ya kuondoka madarakani kwa makosa aliyofanya akiwa ofisini.

Alisema tofauti iliyopo ni kwamba, rais hawezi kushtakiwa kwa makosa ya jinai wakati akiwa madarakani bali anaweza kushtakiwa kwa makosa ya madai hata akiwa madarakani.

Profesa Safari alisema katika nchi nyingi Afrika haamini kwamba hakuna rais aliyepaswa kushtakiwa kwa makosa ya jinai.

Anafafanua kuwa kilichopo ni kitendawili cha nani atamshitaki nani?

“Sioni mwenye uthubutu na uhalali wa kumshtaki mwenzake,” alisema Profesa Safari alipozungumza na The Citizen.

Profesa Safari alisema kimsingi, mtu angeweza kudhani mtu pekee mwenye mamlaka ya kimaadili ya kumwajibisha mwenzake ni yule anayefuata misingi ya uongozi bora na utawala wa sheria, huku akiwa na msimamo usiotiliwa shaka na heshimu katika misingi hii.

“Sasa kama utaniuliza kama tunao watu wa aina hiyo, jibu langu la kweli kabisa litakuwa hapana,” alisema.

Demokrasia ni imani

Mwanasiasa mkongwe nchini, Njelu Kasaka alisema mara nyingi uhuru huanza na mtu mmoja mmoja na kwenda mpaka kwenye taasisi zingine kama Mahakama na Bunge.

Alisema taasisi za kidemokrasia hustawi sehemu ambayo kuna mfumo imara na usiotiliwa shaka wa kidemokrasia.

“Demokrasia ni imani,” alisema Kasaka na kuongeza kwamba, ni lazima kuwepo na watu, viongozi na wananchi, watakaoamini demokrasia ni kitu kizuri na waweze kuuelezea uzuri wenyewe.

“Ikiwa imani hii haitakuwepo basi na demokrasia haitakuwepo. Kilichojitokeza katika nchi hizi -Afrika Kusini, Korea Kusini, Brazil na Ufaransa-ni matokeo ya imani hii (juu ya demokrasia) iliyopo katika maisha ya watu na taasisi,” alisema.

Alisema kukiwa na imani juu ya demokrasia taasisi za kidemokrasia si tu zinahitajika kuanzishwa bali pia kupewa heshima inayopasa.

Demokrasi ni njia si matokeo

Si imani juu ya demokrasia pekee inayofanya utawala wa sheria na uongozi bora kutawala kama katika nchi za Korea Kusini, Brazil, Ufaransa na Afrika Kusini.

Tofauti na nchi nyingine nyingi za Afrika zinazoichukulia demokrasia kama matokeo, wachambuzi wanasema kwa muda mwingi wamekuwa wakiichukulia demokrasia kama njia ya kufikia maendeleo.

Miongoni mwa walio na mawazo haya ni Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo cha Kikatoliki cha Ruaha (Rucu) aliyesema demokrasia imeimarika katika nchi hizo kwa sababu hawajawahi kuitenganisha na maendeleo.

“Nidhamu ya demokrasia ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa,” alisema.