Kiongozi wa baraza la mpito Sudan, Ahmed ajiuzulu siku moja baada ya kuapishwa

Muktasari:

  • Kiongozi wa baraza la mpito Sudan, Ahmed Awadh Auf amejiuzulu kufuatia maandamano ya wananchi wanaodai ni mtu wa karibu wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo,  Omar  al-Bashir aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi

Khartoum, Sudan.Waziri wa ulinzi aliyeapishwa Alhamisi iliyopita kuwa Rais wa Baraza la Mpito la Kijeshi nchini Sudan, Ahmed Awadh Auf amejiuzulu wadhifa huo.

Kufuatia uamuzi huo wa kujiuzulu, nafasi yake ilmechukuliwa na  Jenerali Abdel Fattah al-Burhan Abdulrahman.

Awadh Auf alitangaza hatua hiyo siku moja baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais al-Bashir na yeye kushika hatamu.

Kwenye hotuba yake ya kujiuzulu iliyorushwa kwenye televisheni ya nchi hiyo, Awadh Auf alisema anaachia wadhifa huo kwa maslahi ya taifa na kwa kuwa taifa hilo lina watu wazuri na jeshi la kuaminika.

Alisema  ana imani kwamba makundi hayo mawili yatafanya kazi pamoja. Auf ambaye anakabiliwa na vikwazo kutokana na ushiriki wake kwenye mauaji wakati wa utawala wa al Bashir alikuwa akikabiliwa na shinikizo la kimataifa akitakiwa kuanzisha Serikali ya mpito ya kiraia.

Mapema jana, jeshi liliwahakikishia raia kwamba halina mpango wa kuongoza kwa muda mrefu. Baraza hilo pia lilisema utawala wa kijeshi wa miaka miwili ya mpito unaweza kubadilishwa na kuahidi kwamba linaweza kuvunjwa muda mfupi ujao iwapo kutafikiwa suluhu ya mzozo wa kisiasa unaolikabilia taifa hilo.

Raia walionekana kufurahishwa na hatua hiyo ya ghafla. Awadh Auf alikula kiapo cha kuongoza baraza hilo la mpito usiku wa Alhamisi muda mfupi tu baada ya al- Bashir kupinduliwa na kukamatwa.

Kuondolewa kwa al Bashir kulifuatia miezi kadhaa ya maandamano yaliyokuwa yakiipinga Serikali yake, lakini hata hivyo waandamanaji walisema hawakufurahishwa kuona nafasi yake inachukuliwa na waziri huyo wa ulinzi ambaye ni sehemu ya Serikali yake iliyokaa madarakani kwa miaka 30.

Kundi linaloratibu maandamano hayo lilisema  kupitia ukurasa wa kijamii wa Facebook kwamba kujiuzulu kwa Auf ni ushindi kwa matakwa ya raia.

Aidha, limeijibu hatua hiyo kwa kuapa kwamba waandamanaji wataendelea kusalia mitaani hadi kutakapopatikana Serikali ya kiraia.

Mapema Ijumaa, baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya mkutano wa ndani kufuatia ombi la Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Ubelgiji na Poland.

Balozi wa Ujerumani kwenye Umoja wa Mataifa, Christoph Hausgen aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo kwamba kunatakiwa kuwapo na mchakato wa kisiasa ulio wa haki na jumuishi.

Aidha, alitaka  al-Bashir kupelekwa  Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akisema mataifa yanawajibika kumkabidhi The Hague.

Baraza hilo litakutana tena  Jumatatu kujadiliana kuhusu hali itakavyokuwa nchini humo.