Pierre Bemba arejea rasmi Congo

Muktasari:

  • Atangaza kuongoza maandamano makubwa ya kudai haki na kisha kuombea urais nchini humo

Congo. Mwanasisa maarufu wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Jean pierre Bemba, amerejea nchini humo akitokea uhamishoni mjini Brussels, Ubelgiji na kutangaza maandamano makubwa ya kudai haki.

Mwanasiasa huyo anarejea nchini Congo baada ya kuachiliwa huru na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague alipotumikia kifungo cha miaka 10 gerezani.

Bemba ambaye kwa sasa anaishi nchini Ubelgiji aliwasili nchini humo jana June 23, kwa kutumia ndege binafsi na kupokewa na umati wa watu waliokusanyika katika Uwanja wa ndege wa Kinshasa wakiongozwa na mpinzani Martin Fayulu ambaye aligombea urais kupitia Muungano wa Lamuka.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, kiongozi huyo alisema amepanga kuongoza mfululizo wa maandamano yenye lengo la kudai haki nchini humo ili kuhakikisha anagombea urais wa nchi hiyo.

Awali kiongozi huyo alionyesha azma ya kutaka kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kuungana na Moise katumbi pamoja na Martin Fayulu kupitia muungano wa Lamuka lakini ombi lake lilitupiliwa na Tume huru ya uchaguzi ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, washirika wa Bemba wanadai kwa sasa mwanasiasa huyo amerudi nchini ili kutoa usaidizi kwa mpinzani Martin Fayulu ambaye anasisitiza kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi mkuu uliyopita.

'Mahakama ya katiba inapaswa kuimarisha demokrasi nchini mwetu, badala yake imekuwa kama saratani inayoharibu taasisi zetu. Mmeona jinsi Bunge letu limekuwa na watu ambao hawakuchaguliwa ndio wamelitawala, linachafua jina la nchi yetu ugenini. Sio viongozi tu walio na haki ya kujenga nyumba,” alisisitiza Bemba ambaye alihutubia mamia ya wafuasi wake walifika kumlaki.

Hii ni mara ya pili kwa Bemba kurudi nchini humo. Agosti, 2018 alirejea kwa mara ya kwanza nchini humo na kutangaza azma yake ya kugombea urais.

Kiongozi huyo alikaa gerezani kwa miaka 10 baada ya kupatiana na hatia ya uhalifu uliotekelezwa na wanajeshi wake katika Jamhuri ya Afrika ya kati kabla ya kuondoshewa mashtaka na hatimaye kuachiwa huru baada ya kukata rufaa.

Bemba anarudi nchini Congo wakati Rais Tshisekedi ameingia katika makubaliano ya Serikali ya muungano na Rais Kabila ambaye ana idadi kubwa ya wabunge.