Serikali yagonga nyundo ya mwisho mifuko ya plastiki

Mchuuzi wa mifuko akionyesha mifuko ambayo ni mbadala ya plastiki aliyokuwa ikiiuza katika Mtaa wa Kongo jijini Dar es Salaam jana. Serikali imepiga marufuku uzalishaji, uuzwaji na kutumika kwa mifuko ya plastiki kuanzia tarehe Juni 1, 2019. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ametoa msimamo mkali wa Serikali kuhusu katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki litakaloanza kutumika Juni Mosi, mwaka huu, akisema hakuna muda utakaoongezwa.

“Ndugu zangu hatuongezi muda na Dar es Salaam ndiyo kigezo, mkifanya vizuri hapa, mikoa yote itafanikiwa. Mkoa huu ndiyo msambazaji mkubwa wa mifuko hii.

“Kila mmoja awajibike kuanzia ngazi ya Serikali ya mtaa. Hii ni kazi ya kitaifa hatuwezi kurudi nyuma, hatuwezi kushindwa lazima kila mmoja awajibike.”

Samia alitoa msimamo huo jana alipozungumza kwenye kikao cha viongozi na watendaji wa Dar es Salaam, kuhusu utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki litakaloanza mwezi ujao.

Akihitimisha bungeni bajeti ya ofisi yake Aprili 9, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza marufuku hiyo akibainisha kuwa mifuko hiyo haitakiwi kutumika.

Katika maelezo yake kwa viongozi hao wa Dar es Salaam, Samia alisema hiyo ni mara yake ya pili kushiriki kuzuia mifuko hiyo, kwani aliwahi kushiriki mchakato huo akiwa Waziri wa Biashara na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Bahati nzuri hili ni zoezi langu la pili. Zanzibar inayosifika haina mifuko ya plastiki, tulipiga marufuku nikiwa waziri. Siwezi kuchukua model (muundo) hiyo kusema nimefanikiwa kwa kuwa Zanzibar ndogo, ingawa changamoto ni kuwa mifuko hiyo ilikuwa ikiingia kila pembe,” alisema Samia.

Alisema miongoni mwa waliofanikisha mchakato huo kipindi hicho ni viongozi wa mitaa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi ambao walisimama imara kuona mifuko ya plastiki haingii katika maeneo yao.

Samia alisisitiza kuwa mchakato huo ni wa kitaifa na kila mmoja ana jukumu la kuhamasisha kuachana na matumizi hayo huku akihimiza matumizi ya mifuko mbadala.

“Marufuku hii inaanza Juni Mosi, nataka ijulikane hivyo, ikifika tarehe hiyo hakutakuwa na muda wa nyongeza wala kutazamana. Mifuko ya plastiki ya kubebea bidhaa hatutaki kuiona ikitumika iwe mkononi mwa mtu, sokoni na magengeni au popote.

“Hapatakuwa na kubembelezana, niwatake Watanzania waelewe hayo. Tulishasema sana mwaka huu tutende,” alisema Samia.

Makamu huyo wa Rais alisema mchakato utakwenda sambamba na marufuku ya maji yanayofungashwa kwa mifuko laini ya plastiki maarufu ya ‘kandoro’ aliyosema hayana usalama kwa afya ya binadamu.

Wageni wanaoingia nchini

Akizungumzia wageni wanaoingia na mifuko hiyo nchini kupitia viwanja vya ndege, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema kuanzia Juni Mosi, wageni watakaoingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), watapewa utaratibu maalumu ambao ni pamoja na kukabidhiwa mifuko mbadala.

“Abiria akishuka kwenye ndege akiwa na mfuko wa plastiki atapatiwa elimu kupitia madawati maalumu yatayowekwa eneo la uwanja wa zamani na mpya. Atapewa mfuko mbadala utakaotolewa bure kwa muda wa wiki moja tangu Juni Mosi baada ya hapo, itakuwa ikiuzwa,” alisema Makamba.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema hakuna nguvu itakayotumika wakati wa kutekeleza katazo hilo akisema wakazi wa Dar es Salaam ni waelewa, na kampeni hiyo ni tofauti na ile ya dawa za kulevya.

“Makamu wa Rais hautapata shida ndani ya mkoa huu. Tutakwenda kutekeleza agizo lako vizuri, athari zenyewe zinajulikana, kwa hiyo hakutakuwa na ugumu kwenye mchakato huu,” alisema Makonda.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka aliwataka Watanzania wenye mifuko hiyo kutoichoma moto wala kuitupa chooni, bali tarehe hiyo ikifika waikusanye na kuipeleka eneo maalumu lililotengwa.

Dar yatenga maeneo matatu

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge alisema ili kuhakikisha utekelezaji wa katazo hilo unakwenda kwa ufanisi wameshatenga maeneo ya aina tatu yakayakotumika kukusanyia mifuko ya plastiki.

Alisema eneo la awali litakuwa kwenye kata, likitumika kukusanyia mifuko iliyosalimishwa, la pili litakuwa wilayani litakalopokea mifuko kisha kuipeleka ngazi ya mkoa itakayokusanya mizigo mikubwa.

Ma-Dc wajipanga

Wakuu wa wilaya tano za mkoa huo, wakiongozwa wa Sophia Mjema wa Ilala, walimweleza Samia kuwa wamejipanga ipasavyo katika utekelezaji wa katazo hilo, ikiwamo kuandaa mapipa maalumu yatakayotumika kukusanya mifuko hiyo.