Uganda watua Tanzania kujifunza usajili wa vizazi, vifo

Friday July 19 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Ujumbe wa maofisa sita wa Mamlaka ya Utambuzi na Usajili (NIRA) ya Uganda upo nchini Tanzania kwa  ziara ya siku tano yenye lengo la kujifunza na kubadilishiana uzoefu na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) katika masuala ya usajili wa vizazi.

Katika ziara hiyo, NIRA wamevutia hasa jinsi mpango wa usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka mitano ulivyoweza kutekelezwa kwa mafanikio.

Taarifa iliyotolewa jana Alhamisi na kitengo cha habari cha Rita ilisema maofisa hao mamlaka hizo zinazohusika na usajili zitabadilishana uzoefu.

Akiwasilisha mada kuhusu hali ya usajili wa vizazi na vifo, Meneja Usajili wa Rita, Patricia Mpuya alisema mikakati mbalimbali inaendelea kutekelezwa Tanzania ili kuhakikisha kasi ya kupandisha kiwango cha usajili kinapanda kwani kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi  ya mwaka 2012 ni asilimia 13 tu ya Watanzania walikuwa wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Alisema mpango wa usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwa sasa umeanza na unaendelea kutekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania Bara.

Mpuya alisema mpango huo umekuwa na mafanikio makubwa kwani idadi ya watoto waliosajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa nchini imepanda kutoka asilimia 13.4 mpaka kufikia asilimia 38 ambapo zaidi ya watoto 3.5 milioni wamesajiliwa.

Advertisement

Alisema kupitia mpango huo huduma za usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa zinatolewa bure na  zimesogezwa katika maeneo karibu na makazi ya wananchi na kupatikana katika ofisi za watendaji kata na vituo vyote vya tiba vinavyotoa huduma ya afya ya mama na mtoto.

Kwa upande wake, Mkuu wa ujumbe wa NIRa, Moses Karuhanga aliishukuru RITA kwa kukubali ombi lao la kuja kujifunza masuala ya usajili kwani wanaelewa yapo maeneo ya usajili ambayo Tanzania inafanya vizuri na uzoefu huo vilevile unaweza kuisaidia Uganda.

Ujumbe kutoka Uganda vilevile umetembelea Ofisi ya Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa ( UNICEF) jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Muhimbili na Mkoa wa Iringa katika vituo vinavyotoa huduma za usajili watoto.

Advertisement