VIDEO: Baada ya Maalim Seif kukabidhiwa kadi ya ACT- Wazalendo amesema...

Muktasari:

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na waliokuwa viongozi wa chama hicho leo Jumanne wamekabidhiwa kadi za ACT- Wazalendo

Dar es Salaam. Mwanachama mpya ACT- Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamad ametoa maagizo mawili kwa wanachama wa chama hicho ikiwamo kutokubali kuchokozeka na kupambana kudai demokrasia ya haki kwa busara.

Maalim Seif ameyasema hayo leo Jumanne Machi 19, 2019 mara baada ya kukabidhiwa kadi namba moja ya ACT- Wazalendo na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, katika makao makuu ya chama hicho Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Kadi hiyo namba moja ilikuwa ya mwanasheria wa chama hicho, Albert Msando aliyetimkia CCM.

Maalim Seif amesema anajua wanachama watachokozwa sana, wasikubali kuchokozeka. "Najua mtachokozwa hasa kwenye mitandao ya kijamii, nguvu yao ni kujibizana nao, msikubali kuwapa nafasi hiyo," amesema Maalim Seif huku akiwataka watawale mitandao ya kijamii kwa fikra na mawazo thabiti.

Amewaasa pia kudai haki, demokrasia kwa busara badala ya kutumia nguvu. "Tukitumia miguvu watatumaliza siku moja hawa, tutumie busara zaidi" amesema Maalim aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF kabla ya jana Jumatatu kutangaza kujiunga na ACT-Wazalendo.

Amesema Watanzania wanahitaji kukombolewa hivyo wapambane kwa busara kuhakikisha demokrasia ya haki inapatikana.

Maalim Seif amesema kabla ya kujiunga na chama hicho walipiga hodi kwenye vyama vinne vya siasa ambavyo walikuwa pamoja kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ikiwamo Chadema, NLD, NCCR Mageuzi. Amesema baada ya kupita kote huko, walibaini ACT Wazalendo ndio sehemu sahihi.

Kuhusu mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Maalim Seif amesema hataki hata kumsikia na ameshamalizana naye. "Sitaki kusikia habari zake, mimi na yeye finish (kwisha)" amesema Lipumba.