Chadema watuma mawakili kufuatilia afya ya Mbowe

Dar es Salaam. Chadema imetuma mawakili wake katika Gereza la Segerea kufuatilia afya ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye jana alishindwa kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi inayomkabili, ikielezwa kuwa ni mgonjwa.

Akizungumza na Mwananchi jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema taarifa za kuumwa kwa Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai zimewashtua kwa sababu walikuwa hawajui.

Alisema kutokana na taarifa hiyo wamelazimika kuwatuma mawakili kwenda gerezani ili kujua ni kitu gani kinachomsumbua na kujua kama amepatiwa huduma zinazostahili na kama kuna kitu kinachohitajika.

“Kama hajapatiwa huduma tunataka kujua ni namna gani tunaweza kufanya kwa kushirikiana na watu wa Magereza ili tuhakikishe anarudi katika hali yake ya kawaida,” alisema Mwalimu.

Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, SACP Julius Ntambala alisema hafahamu anachoumwa kwa sababu hiyo ni kazi ya daktari pamoja na wakili wake.

Taarifa za ugonjwa wa Mbowe zilitolewa mahakamani hapo na wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita, wakati kesi ya ya jinai inayomkabili yeye na viongozi wengine wanane wa chama hicho mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ilipotajwa. “Washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako, isipokuwa mshtakiwa wa kwanza (Mbowe) katika kesi hii, ambaye ni mgonjwa na leo (jana) ameshindwa kuletwa mahakamani hapa kusikiliza shauri hili,” alidai Mwita na kuongeza.

“Kwa taarifa tulizopewa na wenzetu wa Magereza ni kwamba mshtakiwa Mbowe ni mgonjwa na leo (jana) ameshindwa kuletwa Mahakamani hapa, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” alidai Mwita.

Wakili Mwita alisema shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani. Baada ya kueleza hayo, hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi, Januari 31.

Mbowe na Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko, wanaendelea kusota rumande kutokana na kufutiwa dhamana.

Mbowe na Matiko, walifutiwa dhamana, Novemba 23, 2018 na Hakimu Mashauri, baada ya kukiuka masharti ya dhamana. Walikata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo wa kufutiwa dhamana, lakini DPP aliweka pingamizi la awali akipinga usikilizwaji wa rufaa hiyo pamoja na mambo mengine, akidai kuwa iko mahakamani isivyo halali kwa kuwa ina kasoro mbalimbali za kisheria.

Hata hivyo, Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Sam Rumanyika ilitupilia mbali pingamizi la DPP na kuamua kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo lakini DPP hakukubaliana na uamuzi huo wa Mahakama na kukata rufaa Mahakama ya Rufani ambayo imepangwa kusikilizwa Februari 18.

Mbali na Mbowe na Matiko, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya msingi ya jinai namba 112/ 2018 ni wabunge wa chama hicho, Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Mnyika (Kibamba), Ester Bulaya (Bunda Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Halima Mdee (Kawe).

Wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na Mwalim.

Salumashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018 katika maeneo ya Dar es Salaam.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika barabara ya Kawawa, Mkwajuni Kinondoni ambalo wanadaiwa kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.