Hivi ndivyo dhamana ya Mbowe, Matiko ilivyoanza na ilikofikia

Moja ya mambo yaliyotikisa katika nyanja ya sheria na siasa wiki lililopita ni sakata la dhamana ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Jinsi sakata la dhamana ya wanasiasa hao wa upinzani lilivyoendeshwa kwa kipindi cha siku tatu mfululizo katika wiki hiyo, ilikuwa kama tamthilia.

Mahakamani kuliibuka majibishano makali ya hoja za kisheria baina ya mawakili wa pande mbili.

Sakata la dhamana ya wawili hao inaanzia nyuma kidogo, Novemba mosi, baada ya Mbowe kutokufika mahakamani Kisutu. Siku hiyo ilipangwa kuwa ya hatua ya awali ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi aliiomba mahakama itoe amri ya kumkamata Mbowe na kumfikisha mahakamani hapo ili aeleze kwanini asifutiwe dhamana kwa kutofika mahakamani.

Hata hivyo, wakili wa akina Mbowe, Peter Kibatala aliieleza mahakama kuwa mdhamini wa mshtakiwa hao, Grayson Celestine alikuwepo mahakamani na angetoa taarifa.

Celestine aliiambia mahakama kuwa aliwasiliana na mke wa Mbowe na kuelezwa kwamba amekwenda nje kwa matibabu kwa dharura kutokana na matatizo ya moyo na shinikizo la damu. Alisema yeye hakuwa ameonana naye, lakini alisema aliondoka akiwa mahututi.

Hakimu Mashauri alimuuliza mdhamini huyo kama ana uthibitisho wowote wa mshtakiwa huyo kusafirishwa nje ya nchi, akajibu kuwa mshtakiwa akirejea angewasilisha vielelezo ingawa aliahidi kuendelea kuwasiliana naye ili avitume kwa njia ya mtandao.

Baadaye Wakili Kibatala alieleza kuwa mdhamini alimueleza kuwa Mbowe alipelekwa Afrika Kusini.

Hata hivyo, Wakili Nchimbi alidai mdhamini hajaonyesha uzito wowote kwa kuwa hajaeleza Mbowe ameenda lini nje ya nchi, nchi gani na hospitali gani na kwamba wanaona huo ni mwendelezo wa dharau kwa mahakama kwa kuwa alishapewa onyo.

Baadaye Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8, akisema iwapo mshtakiwa hatapeleka kielelezo chochote, atatoa amri ya kumkamata ili ajieleze kwa nini asifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti.

Mbowe, Matiko wakamatwe

Novemba 8, Mbowe na Matiko hawakuonekana tena mahakamani, siku ambayo walipaswa kusomewa maelezo ya awali ya kesi

Lakini mdhamini wa Mbowe akaeieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo bado anaendelea na matibabau na kwamba sasa amewasiliana naye anatibiwa Dubai.

Maelezo hayo yalionekana kumshangaza hakimu ambaye alimhoji ni yapi maelezo sahihi kati ya hayo ya Mbowe kutibiwa Dubai na yale ya siku ya kwanza ya kutibiwa Afrika Kusini.

Mdhamini huyo huyo alijibu kuwa hilo la Afrika Kusini hakulitamka kwa mdomo wake.

Dorcas Lugiko, aliyemdhamini Matiko, aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa amekwenda Burundi kikazi na akawasilisha nakala ya tiketi ya ndege na barua ya Bunge ya kumruhusu.

Hata hivyo, Nchimbi alipinga maelezo hayo akisema hayana mashiko, huku wakiikumbusha waliikumbusha mahakama kuwa mdhamini wa Mbowe pia alipaswa kutoa vielelezo vya matibabu.

Kuhusu Matiko, walidai kuwa barua hiyo ya Bunge kumruhusu kusafiri nje ya nchi si kigezo cha kumfanya asifike na kwamba mahakama ni mhimili wenye utaratibu wake.

Hivyo waliomba mahakama itoe amri ya kuwakamata wote na kuwafikisha mahakamani, ombi ambalo hakimu alikubaliana nalo na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 12.

Walivyopambana kujinasua

Novemba 12, Mbowe na Matiko, walifika mahakamani wakiwa na washtakiwa wenzao wengine, kabla hawajakamatwa.

Akijitetea ili asifutiwe dhamana, Mbowe alianza kuelezea mpango wa safari ya Oktoba 28 kwenda Washington DC Marekani kisha Dubai.

Alieleza kuwa alienda alikwenda Washington DC kwenye mkutano wa Oktoba 30, 2018 na kwamba kwa ratiba yake alitarajia kuondoka huko Oktoba 30, usiku na kurejea Dar es Salaam Oktoba 31 kuhudhuria kesi Novemba Mosi, 2018.

Alisema kabla hajaanza safari hiyo aliugua na hivyo asingeweza kufanya safari ndefu ya ndege kwa ushauri wa kitabibu na miiko ya ugonjwa unaomsumbua.

Hakuweza kupata matibabu Marekani kwa sababu bima yake ya matibabu ya kimataifa inaruhusu atibiwe katika nchi za Afrika Mashariki, Afrika Kusini na Dubai.

Alieleza alikwenda Dubai ambako alipata matibabu na akapewa mapumziko na kutakiwa kurejea Novemba 17. Alisema anaugua ugonjwa wa moyo na kwamba aliwasilisha nyaraka zake za safari za matibabu, bima ya matibabu kama uthibitisho mahakamani hapo.

Lakini upande wa mashtaka ulipinga madai hayo, ukisema yanapingana na ya mdhamini wake, jambo ambalo linaonyesha kuna udanganyifu.

Wakili wa Serikali, Jacqline Nyantori alidai kuwa Novemba 2, 2018 Mbowe alikuwa Brussles Ubelgiji ambako alitoka Novemba 6, 2018 kwenda Dubai na kuwasilisha hati ya kusafiria ya Mbowe ikionyesha Novemba 7 alikuwa Dubai na alitibiwa Novemba 8.

Mbowe akana maelezo

Hata hivyo, Mbowe alikana maelezo ya upande wa mashtaka akidai kuwa hakusema anakwenda Marekani kupumzika bali kwa ajili ya mkutano wa kibunge.

Alidai kuwa alitegemea upande wa mashtaka ungesema kuwa haumwi jambo ambalo hawakulisema, lakini akakiri kuwepo Brussles akisubiri tarehe yake ya matibabu.

Utetezi wa Matiko

Kwa upande wake Matiko aliomba msamaha kwa usumbufu uliojitokeza na kwamba hajawahi na hataidharau mahakama.

Alieleza kuwa alimtuma mdhamini wake kumwakilisha mahakamani akiwa na barua ya Bunge ya kumruhusu kusafiri, hoja ambayo ilipingwa na upande wa mashtaka.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Zainabu Mango alidai imekuwa kawaida kwa Matiko kutokufika mahakamani na badala yake kuwasilisha nyaraka na wadhamini tu.

Baada ya kusikiliza utetezi wao, Novemba 23, mahakama iliwafutia dhamana wawili hao.

Hakimu Mashauri alikubaliana na hoja za upande wa mashtaka akisema kuwa kilichofanywa na washtakiwa hao ni kudharau amri za mahakama kwa makusudi.

Watangaza azma ya kukata rufaa

Wakili wa utetezi, Kibatala hakuridhika na uamuzi huo, hivyo wakatangaza nia ya kukata rufaa Mahakama Kuu na kuomba mahakama isimamishe usikilizwaji wa kesi hiyo.

Wakati mahakama ikiandaa uamuzi kuhusu kusimamisha usikilizwaji wa kesi hiyo, mawakili wa washtakiwa walitumia muda huo mfupi kukata rasmi rufaa na kuiwasilisha mahakamani.

Hakimu alisema hangeendelea na shauri hilo hadi Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa rufaa ya washtakiwa hao.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6 na Desemba 7 alikubaliana na hoja za kina Mbowe za kusikiliza rufaa, lakini Serikali ikakata tena rufaa Mahakama ya Rufani na hivyo wawili hao kuendelea kuwa mahabusu hadi sasa.