JPM amtaka waziri kuhamia kwenye pagale

Sunday April 14 2019

Jengo la Wizara ya Ofisi ya Rais (Tawala za

Jengo la Wizara ya Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) linalojengwa katika Mji wa Serikali jijini Dodoma. Rais John Magufuli amesema wizara hiyo imeshindwa kukamilisha ujenzi wa ofisi hizo kwa muda uliopangwa hivyo amemtaka Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo na watumishi wa wizara hiyo kuahamia hivyo hivyo.Picha na Edwin Mjwahuzi. 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayoongozwa na Seleman Jafo kuhamia katika jengo la ofisi yao ‘pagale’ ambayo haijakamilika hivyo hivyo.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana ikiwa ni muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kueleza kuwa alikuwa na makubaliano na mawaziri kuwa siku majengo hayo yakizinduliwa mawaziri wangehamia.

Hata hivyo, Majaliwa alimweleza Rais kuwa kuna baadhi ya wizara ikiwemo Tamisemi ambazo majengo yao yamechelewa kukamilika kutokana na kuchelewa kupata fedha.

Waziri Mkuu alitaja muda ambao majengo hayo yatakamilika ni mwishoni mwa Aprili huku jengo la Tamisemi likielezwa litakuwa tayari mwishoni mwa Mei kutokana na ramani yake kuwa tofauti na majengo mengine.

Hata hivyo, Rais Magufuli alisema hataki kusikia kunakuwa na kisingizio cha majengo mengine kuwa hayajakamilika na badala yake kama mtu ameshindwa basi akae hata chini ya mwembe ili mradi awe Mtumba ambako ndiko mji wa kiserikali uliko.

“Kwa upande wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambao jengo lao halijakamilika kwa sababu walitaka kujenga ghorofa, naagiza ifikapo Jumatatu (kesho) nao wahamie humohumo, wakabebe viti kule waje hapa maana tukisema wengine watakuja haiwezekani watu watabaki mjini,” alisema Magufuli

Advertisement

Kiongozi huyo alisema muda wote atakapokuwa anawahitaji mawaziri, hakuna sababu ya kuwaita bali atawafuata kwenye majengo hayo hivyo akaomba kila mmoja wao ahamie kwa vitendo siyo maneno.

Kwa upande mwingine aliwataka wakazi wa eneo hilo na mji kwa ujumla kutumia nafasi ya uwepo wa wizara katika kuchangamkia fursa ikiwemo kujenga migahawa na sehemu za vinywaji huku akiahidi kupeleka Sh4 bilioni kujenga kituo cha afya ndani ya mji huo ambayo itahudumia na wakazi wa maeneo jirani.

Advertisement