Jalada la tuhuma za mauaji ya Naomi mezani kwa DPP

Tuesday July 23 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jalada la tuhuma za mauaji dhidi ya Naomi Marijani anayedaiwa kuuwawa na kuchomwa moto na mumewe, limetua ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kati ya jana au leo.
Naomi anadaiwa kuuwawa na mumewe Khamis Luwonga kisha kumchoma moto na majivu yake kuyafukia shambani kwake lililopo  katika kijiji cha Marogoro wilayani Mkuranga.
Akizungumza na Mwananchi jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa upelelezi wa Kanda maalum ya Dar es Salaam, Camilius Wambura alisema jalada hilo litafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa kanda hiyo kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
“Ninachoweza kueleza kwa kifupi ni kwamba tunafikiria kuliwasilisha jalada kwa mkurugenzi wa mashtaka leo (jana) au kesho (leo) kwa hatua zaidi,” amesema Wambura jana.
Naomi alitoweka nyumbani kwake Mei 15 mwaka huu , siku 63 baadaye, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kuwa Luwongo ambaye ni mumewe, amekiri kumuua na kumchoma moto kisha kufukia majivu yake.
Taarifa hiyo ya polisi iliyotolewa Julai 17, mwaka huu, ilileza kuwa Luwongo aliwaongoza askari kwenda kufukua na kupata mabaki yaliyochukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha vinasaba (DNA).
Kwa mujibu wa polisi, majibu ya kipimo hicho ndiyo yatakayothibisha kwamba mabaki na majivu hayo ni ya Naomi au la.
Zimepita siku sita tangu taarifa hiyo itolewe na familia ya Naomi ikishindwa kuweka msiba kwa kusubiri majibu ili iweze kuzika mabaki hayo ya mwili wa ndugu yao.
Kaka wa Naomi, Wiseman Marijani amesema familia yao haina budi kusubiri kwa kuwa wanachotaka ni kuona haki dhidi ya ndugu yao inatendeka.
“Kama tuliweza kuwa wavumilivu kwa zaidi ya siku 60 tukiwa hatufahamu lolote kuhusu ndugu yetu alipo, hatuwezi kushindwa sasa.
“Hatuamini kama zoezi la kupima sampuli litachukua siku 60 nyingine, tutavumilia ili hili la kisheria likamilike ili haki itendeke na wahusika wawajibishwe,” amesema Wiseman.
Akijibu kuhusu kinachoendelea, Wambura amesema, “hayo ni mambo ya uchunguzi, hatuwezi kuwa tunasema kila kitu.”

Advertisement