VIDEO: Jinsi Mbowe na Matiko walivyoachiwa kwa dhamana

Muktasari:

Ni wabunge wa Chadema, Freeman Mbowe na Ester Matiko ambao wamekaa mahabusu kwa siku 104, ambapo Jaji wa Mahakama Kuu amesema inahitaji sababu nzito ili kufuta dhamana ya mshtakiwa yeyote

Dar es Salaam. Tangu walipoingia gerezani Novemba 23 mwaka jana, Freeman Mbowe na Esther Matiko wamekuwa wakipelekwa na kuondolewa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza.

Walipata fursa ndogo ya kuongea na mawakili wao na baadaye kuongozwa hadi kwenye gari la Jeshi la Magereza kwa ajili ya kurejeshwa mahabusu.

Lakini baada ya siku 104, jana hali ilikuwa tofauti; waliingia kwa ulinzi mkali, wakatoka bila ya ulinzi na kupata muda wa kutosha, si tu wa kuongea na mawakili wao, bali na mashabiki na wafuasi wengine wa Chadema waliokuwa ndani na nje ya Mahakama Kuu.

Kitu kimoja kilichoonekana kutobadilika wakati wote walipoingia na kutoka mahakamani na ambacho kiliendelea jana, ni tabasamu katika nyuso za Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema na Matiko (mbunge wa Tarime Mjini).

Hiyo ilikuwa baada ya Jaji Sam Rumanyika kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ya kuwafutia dhamana wawili hao kwa kosa la kukiuka masharti waliyopewa.

Hali kama hiyo ilikuwa mkoani Morogoro ambako wabunge wawili, Peter Lijualikali na Susan Kiwanga walipata dhamana, lakini wakarejeshwa mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti.

Mbowe na Matiko walikata rufaa kupinga uamuzi wa kuwafutia dhamana uliofanywa na Hakimu Wilbard Mashauri.

Katika hukumu yake, Jaji Rumanyika alisema ni msingi wa kisheria kwamba kufutwa kwa dhamana ya mshtakiwa huja baada ya mahakama kutwaa fungu la dhamana ya mshtakiwa endapo mshtakiwa ataruka dhamana.

Alisema mdhamini ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani kwa tarehe anayohitajika na au kutoa maelezo pale mshtakwa anaposhindwa kufika mahakamani, na hivyo alitakiwa apewe nafasi ya kuulizwa kwa nini fungu lake lisichukuliwe.

“Kwa kuwa katika shauri hili wadhamini hawakutoa sababu ni kwa nini fungu lao la dhamana lisitwaliwe, si tu uamuzi huu wa kuwafutia dhamana warufani si sahihi, bali pia ulitolewa kabla ya wakati,” alisema Jaji Rumanyika

“Ninaamuru warufani waachiwe huru mara moja isipokuwa kama wataendelea kushikiliwa kisheria kwa sababu nyingine.

“Na ninaamuru jalada la kesi hii lirudishwe Mahakama ya Hakimu Mkazi mara moja ili kesi ya msingi iweze kuendelea kwa haraka sana.”

Uamuzi huo uliibua shangwe za furaha kwa wanachama wa chama hicho ndani ya ukumbi wa mahakama huku wafuasi waliokuwa nje wakiimba “people’s power” ambayo ni kaulimbiu ya Chadema.

Si tu makelele hayo ya furaha, pia waliwazonga wabunge hao huku kila mmoja akitaka ama kuwakumbatia au hata kuwashika mkono wa kuwafariji, hali kadhalika kwa mawakili wao, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya.

jaji Rumanyika pia alishangaa kwa uamuzi huo kutolewa miezi mitatu baada ya warufani kuwasilisha shauri lao kwa hatia ya dharura. “Hii ni moja ya rufaa za ajabu sana,” alisema Jaji Rumanyika wakati akisoma hukumu yake.

“Pamoja na kwamba rufaa hii ilikatwa kwa hati ya dharura, ni bahati mbaya kwamba haikuweza kuamuriwa mpaka leo miezi mitatu baadaye kwa sababu kulikuwa na rufaa na mapingamizi.”

Pamoja na kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, Jaji Rumanyika pia alizungumzia haki ya dhamana na namna ya kushughulika nayo.

Pia, Jaji Rumanyika aliwapunguzia mzigo wa masharti ya dhamana waliyopewa kwa kuwataka waripoti mahakamani kila mwisho wa mwezi, badala ya kuripoti kituo cha polisi kila Ijumaa.

Kauli nzito za Jaji Rumanyika

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Rumanyika alikubaliana na hoja za Kibatala na Mtobesya kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kufuta dhamana kwa kuwa haikufuata misingi na matakwa ya kisheria.

Alisema ni msingi wa kisheria kwamba kufutwa kwa dhamana hufuata baada ya mahakama kutwaa fungu la dhamana endapo mshtakiwa hatakuwa akifika mahakamani.

Alisema hii ni kwa sababu jukumu la kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani kwa tarehe anayohitajika na au kutoa maelezo pale mshtakiwa anaposhindwa kufika mahakamani ni la mdhamini.

Hivyo, alisema kabla ya mahakama kumfutia mshtakiwa dhamana lazima kwanza mdhamini apewe nafasi ya kujieleza kuhusu kutwaliwa kwa fungu lake na iwapo mshtakiwa ataendelea kutoonekana ndipo litwaliwe na iwapo hataonekana, ndipo dhamana ifutwe.

Jaji Rumanyika pia alikubaliana na hoja za mawakili wa Serikali kuwa kitendo cha washtakiwa kufika wenyewe mahakamani kabla ya kukamatwa kama mahakama ilivyoamuru, si hoja ya msingi kama mawakili wa utetezi walivyodai.

Lakini aliigeukia Mahakama ya Kisutu kuwa baada ya washtakiwa hao kufika mahakamani, ilipaswa kufahamu na kujihakikishia kuwa sasa si wapotevu tena na akasisitiza kuwa kwa msingi huo, dhamana zao hazikupaswa kufutwa.

Hata hivyo, alitahadharisha hiyo haina maana kwamba washtakiwa waendelee kukaidi mahakama kadri wanavyoona kuwa matakwa yao yanatimizwa.

Akizungumzia dhana ya dhamana na namna ya kuishughulikia, Jaji Rumanyika alisema pamoja na kwamba majaji na hakimu wana mamlaka ya kuamua dhamana hata kwa utashi wao, uamuzi ni lazima uzingatie misingi ya kisheria.

Alisema inaweza kuwa ni kinyume cha sheria kutoa dhamana bila kuweka sababu, lakini ni kinyume cha sheria na hatari kumnyima dhamana na hatari zaidi kumfutia mshtakiwa dhamana bila sababu za msingi. “Dhamana ni faraja ya kimahakama (kwa mshtakiwa) ambayo yule aliyeitoa hawezi kuichukua tu kwa matakwa yake,” alisema Jaji Rumanyika.