Breaking News

Kamati ya Bunge yamhoji CAG dakika 156 Dodoma

Tuesday January 22 2019

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge walipokaa kikao kwa ajili ya kumhoji Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad jijini Dodoma jana. Picha ndogo Profesa Assad (kulia) akiingia bungeni kuhojiwa na kamati hiyo. Picha na Habel Chidawali 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge jana ilitumia dakika 156 kumhoji Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad aliyeitwa mbele ya kamati hiyo kueleza kauli yake kuhusu “udhaifu wa Bunge.”

Profesa Assad aliyefika katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma saa 4:47 asubuhi akiwa katika gari jeupe lenye namba STK 6249 bila msaidizi yeyote, alikuwa amebeba begi dogo jeupe huku akionekana kuwa makini.

Profesa Assad aliitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa wakati alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) akiwa New York, Marekani alikokuwa akihudhuria mkutano.

Alitumia neno “udhaifu” wa Bunge alipokuwa akieleza sababu za kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake ambazo zimekuwa zikibainisha ufisadi.

Ilivyokuwa Dodoma

Jana baada ya Profesa Assad kuingia getini alipokelewa na askari kanzu wa Bunge na kuelekezwa lango la kuingilia na kama utaratibu wa siku zote alikaguliwa na kupewa kitambulisho cha wageni badala ya kile cha VIP ambacho maofisa hutumia siku zote.

Advertisement

CAG ambaye wakati wote alionekana mwenye uso wa furaha, alielekezwa na maofisa kwenda kuketi katika eneo ambalo wageni huwa wanakaa kisha akapelekewa kitabu cha wageni na Katibu wa Spika, Said Yakubu.

Maeneo yote ulinzi ulikuwa mkali kwa askari kanzu, lakini tofauti na siku zote, waandishi wa habari pekee ndiyo walikuwa na nafasi ya kumsogelea na kumpiga picha.

Aitwa ukumbini

Profesa Assad alifutwa na mmoja wa maofisa na kumuomba aingie ukumbini saa 5:03 asubuhi na dakika mbili baadaye alikuwa ameshaingia katika ukumbi huo na kusalimiana na wajumbe wa kamati hiyo akiwemo mwenyekiti wake, Emmanuel Mwakasaka, kisha akawasha kompyuta yake mpakato (laptop) iliyokuwa ndani ya begi.

“Ndugu zangu shahidi wetu yuko mbele ya kamati yetu, tunamshukuru sana kwa kukubali wito wetu kama ambavyo tulimpa samansi yetu. Kwa sasa niwashukuru sana ndugu waandishi wa habari kwa ushirikiano wenu lakini naomba sasa mtupishe,” alisema Mwakasaka ambaye ni mbunge wa Tabora Mjini (CCM).

Mahojiano na mapumziko

CAG alipoingia hali ilikuwa tulivu na hakuna mjumbe aliyekuwa akitoka nje hadi ilipofika saa 6:45 mchana alipotoka nje kupumzika kabla ya kuitwa tena ukumbini saa 7:15 mchana.

Saa 7:57 mchana, CAG alitoka tena kupumzika na wajumbe walionekana wakitoka na kuingia kisha akaitwa tena saa 8:35 mchana na kukaa katika ukumbi huo kwa dakika 12 tu kutokana na kutoka saa 8: 47 na kusindikizwa na askari kanzu hadi nje huku waandishi wakizuiwa kuzungumza naye.

Kauli ya mwenyekiti

Mara baada ya kutoka, Mwakasaka na makamu wake, Dk Christine Ishengoma waliita waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa, CAG alitoa ushirikiano mzuri na alijibu maswali yote aliyoulizwa.

Mwakasaka alisema kamati hiyo ilikuwa imemaliza kazi yake jana na kusubiri kukamilisha taarifa yake ambayo itapelekwa kwa Spika wa Bunge kwa ajili ya uamuzi mwingine.

“Shahidi wetu ametoa ushirikiano mkubwa sana, tumemhoji ametujibu maswali yetu kama alivyoulizwa na sasa tunapeleka hatua ya pili ambapo taarifa itakwenda kwa Spika kwa hatua nyingine,” alisema Mwakasaka huku akikataa kufafanua siku watakayopeleka taarifa hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema leo asubuhi kamati hiyo itakutana tena kwa ajili ya kumhoji mbunge wa Kawe, Halima Mdee kama ilivyoagizwa na Spika Job Ndugai.

Wajumbe wa kamati

Mbali na Mwakasaka na Ishengoma, wajumbe wengine wa kamati waliokuwapo jana ni George Lubeleje, Shamsi Vuai Nahodha, Agustino Masele, Rose Kamili Sukum, Hassan King, Alan Kiula na Ruth Molell.

Wengine ni Almas Maige, Ramo Makani, Omari Kigua, Mariam Kisangi, Adadi Rajabu, Prosper Mbena na Magreth Sita. Wajumbe hao walikuwepo ukumbini wakati CAG akiingia kuhojiwa.

Tofauti na wengine

Kwa nyakati kadhaa kumekuwa na mahojiano ya baadhi ya viongozi wanaotoka nje ya mhimili wa Bunge wakiwepo wakuu wa mikoa, wilaya, wahariri na watu wengine, hata hivyo jana kulikuwa na tofauti kidogo.

Mara nyingi mahojiano hufanywa kwa siri kubwa huku wanahabari wakizuiwa kufanya chochote hata kuwapiga picha wanapoingia au kutoka zaidi ya kutegemea picha kutoka ofisi ya Bunge.

Hali ilikuwa tofauti jana kwani kila hatua iliyofanyika kulikuwa na taarifa za kutosha kuhusu ambacho kingefanyika baada ya hatua moja kufanyika.

Leo zamu ya Mdee

Leo kamati hiyo itamhoji mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ambaye aliunga mkono kauli ya CAG kuhusu Bunge. Akizungumza na Mwananchi jana Mdee alisema, ““Siku hizi wabunge tuna dharaulika sana, tunanyang’anywa ofisi, tunakamatwa hovyo na hakuna kiongozi wa Bunge anayejitokeza kuzungumzia, kwa hiyo nina hoja kama 20 ambazo zitakwenda kuziwasilisha kwenye kamati.”

Advertisement