Kigogo Chadema auawa nyumbani, azikwa

Malinyi. Uongozi wa Chadema mkoa wa Morogoro umeeleza kusikitishwa na kifo cha katibu mwenezi wa jimbo la Malinyi, Lucas Lihambalimu baada ya kudaiwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani usiku wa manane.

Akizungumza na Mwananchi jana, katibu wa Chadema mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola alisema kwa mujibu wa taarifa walizopata watu wasiojulikana walifika nyumbani kwa Lucas saa 8:00 usiku na kumgongea.

Okola alisema alipofungua mlango ghafla alipigwa na kushambuliwa na watu hao kwa kumpiga risasi shingoni.

“Kihistoria Lucas hakuwa na ugomvi na mtu au watu alikuwa mpole na mchapa kazi ndani ya chama, tuliposikia ameuawa kila mtu alipigwa butwaa,” alisema.

Pia, katibu huyo alisema kwa sasa wanasubiri uchunguzi wa polisi. Mazishi ya katibu huyo mwenezi yalifanyika juzi wilayani Malinyi. Marehemu ameacha mke na watoto.

Hata hivyo, jitahada za kumpata kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa baada ya mwandishi aliyefika ofisini kwake kuelezwa na msaidizi wake kuwa anaumwa.