Kinyago kutumika kuinua elimu Mtwara

Saturday December 29 2018
pic kinyago

Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara,Moses Machali (mwenye nyeusi) na mbunge wa Nanyumbu,Dua Nkurua wakifurahia zawadi ya kinyago,kushoto ni mkuu wa mkoa,Gelasius Byakanwa.Picha na Haika Kimaro

Mtwara. Mkoa wa Mtwara katika kuhakikisha unafanya vizuri katika elimu umeanzisha utaratibu wa kugawa zawadi ya kinyago kwa wilaya inayofanya vibaya kwa ngazi ya mkoa.

Kutokana na wilaya ya Nanyumbu kuwa ya mwisho kimkoa katika matokeo ya darasa la saba kwa mwaka huu, mkuu wa mkoa huo, Gelasius Byakanwa tayari ameukabidhi uongozi wa wilaya kinyago hicho kwa lengo la kuwakumbusha na kutilia mkazo suala la elimu.

Kinyago hicho kimetolewa leo Jumamosi Desemba 29, 2018 katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) baada ya mbunge wa Mtwara vijijini (CCM), Hawa Ghasia kupendekeza na kusema katika jimbo lake tayari walishaanza kukigawa kwa shule inayofanya vibaya.

Akizungumza mkuu wa wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali baada ya kukabidhiwa kinyago hicho chenye sura nyeusi na watu waliokaa kwa masikitiko amesema kitawafanya wazidi kuweka mkazo lakini mwakani watakigawa kwa wilaya nyingine.

Amesema licha ya wilaya hiyo kuongeza kiwango cha ufaulu kwa asilimia 20 kutoka asilimia 51 ya mwaka juzi hadi asilimia 72 ya mwaka huu bado wamekuwa wa mwisho kutokana na sababu mbalimbali lakini juhudi za kuinua elimu zinaendelea kama ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu.

Machali aliyewahi kuwa mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi) amesema hatua zaidi walizochukua ni pamoja na kuwasiliana na Tamisemi ili kuwaongezea walimu lakini pia baada ya idara ya udhibiti wa elimu wamefanya ukaguzi katika shule na kugundua baadhi ya walimu wanafundisha bila maandalizi ya masomo sambamba na tatizo la utoro.

Advertisement

"Tumefanya mabadiliko kwa baadhi ya walimu wakuu kama mkakati kuhakikisha tunakuwa na walimu wanaozitambua nafasi zao na kuzitendea haki na kuhakisha wanatoa taaluma safi kwa wanafunzi," amesema Machali.

Katibu tawala wa wilaya hiyo, Salum Palango amesema bado changamoto iliyopo ni upande wa baadhi ya wazazi kwa sababu wapo wazazi wanaopenda watoto wao wafeli lakini kwa sasa wameweza kuwadhibiti.

Advertisement