VIDEO: Kiwanga, Lijualikali, wenzao saba warudi rumande
Muktasari:
- Wabunge hao wanashitakiwa kwa makosa manane likiwemo la kuharibu mali kwa kuchoma moto majengo ya serikali ya kijiji cha Sofi wilayani Malinyi kwa kile kinachodaiwa kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Sofi.
Morogoro. Wabunge wa Chadema Suzan Kiwanga wa jimbo Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero na wafuasi saba wa chama hicho wamerudishwa rumande hadi Machi 4.
Uamuzi huo umefikiwa na mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro iliyoridhia ombi la upande wa Jamhuri la kuwaongezea muda ili waweze kuwasilisha kiapo cha nyongeza cha kupinga dhamana ya washtakiwa hao.
Washtakiwa hao wamekaa ndani kwa wiki moja sasa tangu walipofikishwa mahakamani hapo mara ya kwanza Februari 25 na leo walifikishwa tena mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha.
Kabla ya kutoa uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo ya jinai namba 43 ya mwaka 2019, hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Elizabeth Nyembele alipokea hoja kutoka upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa Serikali Neema Haule na upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Bathelomew Tarimo.
Wakati wakiwasilisha hoja hizo uliibuka mvutano mkali wa kisheria baina ya upande wa Jamhuri na upande wa utetezi na hivyo Hakimu Nyembele aliamua kuahirisha kesi hiyo kwa muda wa dakika 15 ili kupitia hoja zote.
Baada ya kupitia hoja hizo, baadaye alikubali ombi la upande wa Jamhuri la kuongeza muda kwa ajili ya kuwasilisha kiapo cha nyongeza cha kupinga dhamana ya washtakiwa hao kwa kuzingatia kuwa muda uliotolewa awali ulikuwa mchache.
Baadhi ya hoja za kisheria walizokuwa wakivutana mawakili hao ni pamoja na sababu za kushindwa kuwasilisha kiapo hicho kwa wakati ambao upande wa Jamhuri ulidai kuwa mtu anayehusika kusaini kiapo hicho ambaye ni SP Rashidy Njiku amesafiri kwenda Kilosa kikazi.
Akikazia hoja hiyo Wakili wa Jamhuri, Neema Haule amedai kuwa si kila mtu anaweza kusaini kiapo hicho bali yupo mtu mwenye mamlaka ya kukisaini na kwamba hawana nia yoyote ya kuchelewesha kesi hiyo.
Wakili wa utetezi Tarimo amedai kuwa kitendo wanachokifanya upande wa Jamhuri kinaionyesha wazi mahakama kuwa hawana nia ya kuwasilisha kiapo hicho cha pingamizi la dhamana na hivyo aliiomba mahakama kutowasikiliza.
Mapema wakifikishwa mahakamani hapo mbunge Kiwanga alionekana akitembea bila ya viatu (peku) baada ya kandambili zake kumpa mshtakiwa mwenzake hata hivyo kabla ya kurudishwa rumande wanachama wa Chadema walimnunulia kandambili mpya.
Wakati Kiwanga na wenzake wakiingia mahakamani hapo alisikika akiwaambia wanachama hao kuwa wasiwe na wasiwasi wako salama na wanaendeleza mapambano.
“Watu wa Chadema msiwe na wasiwasi tuko vizuri, tuko salama kabisa, mahabusu ya magereza ni sehemu salama si kama polisi,” alisema Kiwanga.