VIDEO: Kusaga kutoa ratiba ya mazishi ya Ruge

Muktasari:

Amshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kuwasaidia katika kumuuguza Ruge Mutahaba

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga amesema kesho Jumatano asubuhi Februari 27,2019 watatoa ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa kampuni hiyo, Ruge Mutahaba.

Ruge amefariki dunia  Februari 26, 2019 nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza na Mwananchi, Mikocheni jijini Dar es Salaam usiku huu ulipo msiba, amesema kutakuwa na kikao usiku huu na kesho asubuhi taratibu zote zitawekwa wazi.

“Tutakaa kupanga kuhusu mazishi ya mpendwa wetu halafu asubuhi tutawajulisha,” amesema.

Kusaga amemshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli, Serikali na Watanzania kwa ujumla kwa ushirikiano waliowapa katika kipindi cha kumuuguza Ruge.

“Tunamshukuru Rais na Serikali yake bila kuwasahau Watanzania kwa ujumla wao kwa upendo waliotuonyesha katika juhudi za kuokoa uhai wa mpendwa wetu lakini ndiyo hivyo mapenzi ya Mungu yametimia,” amesema Kusaga.