VIDEO: Lowassa afunguka hatima yake Chadema

Muktasari:

  • Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani amefunguka kuhusu hatima yake ndani ya Chadema akieleza kuwa hana mpango wa kukihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania huku akiwakumbuka wananchi walimpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
  • Lowassa alishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo nyuma ya Rais John Magufuli.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amefunguka kuhusu hatima yake ndani ya Chadema na kusisitiza kuwa hana mpango, hajafikiria wala hajapanga kuondoka katika chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

“Sina mpango wa kuondoka Chadema, sijapanga wala sijafikiria kuondoka Chadema,” alisema Lowassa alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi ofsini kwake jijini Dar es Salaam jana.

Lowassa alizungumza na Mwananchi kwa mara ya kwanza baada ya viongozi wa chama hicho kumtaka ajitokeze na kuweka wazi msimamo wake.

Mwanzoni mwa wiki hii, naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alimtaka Lowassa kujitokeza kuweka msimamo wake hadharani baada ya kusifiwa mara kwa mara na viongozi wa juu wa CCM na Serikali.

“Siasa maneno mengi siku hizi, kila mahali maneno.. maneno,” ndivyo alivyoanza kujibu Lowassa alipoulizwa kuhusu madai kuwa ana mpango wa kurejea CCM.

“Ningetaka kuweka wazi kwa Watanzania na wanachama wa Chadema kwamba sina mpango wa kuondoka Chadema hata kidogo, sina mpango wa kuondoka Chadema, sijapanga wala sijafikiria kuondoka Chadema,” alisema Lowassa aliyezaliwa miaka 65 iliyopita wilayani Monduli.

Waziri huyo mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne alisema, “Ninazo sababu nyingi, katika uchaguzi uliopita walionibeba ni Chadema na walinibeba tukazunguka na tukapeperusha bendera zetu nchi nzima vizuri na kwa umakini na tukapata watu waliotuamini.”

Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza kuhamia upinzani katika historia ya Tanzania, alisema anakosa sababu ya kuwaambia watu milioni sita waliompigia kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Katika uchaguzi huo aligombea nafasi ya urais kupitia muungano wa vyama vinavyounda Ukawa (Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD) na kupata kura 6,072,848 (sawa na asilimia 39.97) akiwa nyuma ya Rais John Magufuli aliyeshinda kwa kupata kura 8,882,935 (asilimia 58.46).

“Watu wale zaidi ya milioni sita ndizo kura wanazokubali Tume ya Uchaguzi, watu wale zaidi ya milioni sita nawaambia nini? Nawaambia naondoka Chadema kwa sababu gani? Kwa hoja gani?” alihoji.

Lowassa ambaye ameshika nafasi mbalimbali katika serikali za awamu nne za mwanzo, alitoa matumaini zaidi kwa viongozi na wanachama wa Chadema. “Tumepigana pamoja, tunangojea kupangana kupigana pamoja kwenye uchaguzi ujao, anayesema ninataka kuondoka Chadema anajifurahisha, nataka kuwahakikisha wanachama wa Chadema na wananchi nipo Chadema na nitaendelea kuwa Chadema, naomba waendelee kuniunga mkono nikiwa Chadema,” alisema huku akirudia mara kwa mara kutaja jina la chama chake.

Kusifiwa na viongozi CCM

Alipoulizwa kuhusu viongozi wa CCM na Serikali kumsifu mara kwa mara, alisema, “Naacha wananchi wahukumu na wenyewe wahukumu, mimi naamini ni nia njema na nia njema itaendelea kuwepo.”

Alipoulizwa haoni kama kusifiwa huko na viongozi wa CCM na Serikali kunaweza kutafsiriwa tofauti, alisema: “Anayetaka kufikiria hivyo ni hiyari yake, huwezi kumnyima binadamu kufikiria, ila ninachosema mimi sina mpango wa kuondoka Chadema.”

Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amekuwa akimmwagia sifa Lowassa akimuelezea kuwa kiongozi mzalendo wa kweli, mstaarabu aliye tofauti na viongozi wengine wa upinzani.

Hivi karibuni wakati akizindua maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Magufuli alirudia tena sifa hizo, akisema Lowassa ni mwanasisasa mstaarabu ambaye baada ya kushindwa mbio za urais 2015 alikubali matokeo. Alimtaka awashauri watu anaowaongoza watulie, akisema la sivyo wataishia gerezani. Siku hiyo, Lowassa alimpongeza pia Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya.

Julai mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na viongozi wakuu wastaafu Ikulu Dar es Salaam, pia alitoa sifa kama hizo kwa Lowassa akimuita kuwa ni “mtu mwema sana” ambaye hakuwahi kumtukana.

Mwanzoni mwa wiki hii, sifa hizo zilidakwa na katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliyesema Lowassa hana unafiki kwa sababu aliondoka ndani ya chama hicho baada ya kukosa ridhaa ya kugombea na kwenda chama kingine (Chadema) badala ya kubaki ndani kinafiki na kuwagawa wanachama.

Sifa anazomwagiwa Lowassa na viongozi wakuu wa CCM zimekuwa zikiibua mijadala na wakati mwingine maswali, baadhi wakihisi kuwa chama hicho kinamhofia na wengine wakidhani jina lake linatumika kuwagawa wapinzani.

Jambo hilo lilimfanya naibu katibu mkuu wa Chadema - Zanzibar, Mwalimu kumtaka Lowassa kujitokeza na kuweka msimamo wake hadharani.

Lakini katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema anaamini CCM wanamtumia Lowassa kuwafarakanisha. Alisema (CCM) wanajua Lowassa ana nguvu kubwa akiwa upinzani kama ilivyoonekana kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita na ndiyo maana wanajaribu kumdhoofisha.

Dk Mashinji alisema bado wanaendelea kumuamini Lowassa na yumo kwenye mipango yao.