Mahakama yatupa kesi ya kupinga adhabu ya kunyonga

Muktasari:

Harakati za wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole kuleta mabadiliko yenye lengo la kumpa nafuu ya adhabu mshtakiwa anayetiwa  hatiani kwa kosa la mauaji  zimeshindikana baada ya Mahakama Kuu Dar es Salaam kumkatalia hoja zake katika kesi aliyoifungua iamuru kuwa mtu anayetiwa hatiani kwa kosa hilo apewe nafasi ya kujitetea badala ya kumhukumu kifo moja kwa moja.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya kikatiba ya kupinga adhabu ya kunyonga kama sharti la lazima kwa washtakiwa wanaotiwa hatia kwa makosa ya mauaji.

Hukumu ya kesi hiyo imetolea jana Alhamisi Julai 18, 2019 na jopo la majaji watatu; Ama-Isario Munisi, Dk Benhajj Masoud na ElinazerLuvanda  kutokana na kutokukubaliana na hoja zilizotolewa na wa mdai katika kesi hiyo.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 22 ya mwaka 2018 ilifunguliwa mwaka 2018 na Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kupitia kwa wakili, Jebra Kambole.

Katika kesi hiyo, Kambole alikuwa anapinga kifungu cha 197 cha Kanuni za Adhabu (Penal Code- PC), Sura 16, marekebisho ya mwaka 2002.

Alikuwa akidai kuwa kifungu hicho kinakinzana na katiba ya nchi kwa kuwa  kinatoa sharti la lazima la adhabu ya kunyongwa kwa mtu aliyetiwa hatiani kwa kosa la kuua kwa kukusudia.

Kambole alikuwa akiiomba mahakama iamuru kifungu hicho kiondolewe katika sheria za nchi na Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wake (AG) kuwasilisha marekebisho ya masharti ya kifungu hicho na kuandaa mwongozo wa utoaji adhabu mbadala.

Pia,  alikuwa anaiomba mahakama iamuru watu ambao tayari wameshatiwa hatiani kwa makosa ya mauaji sharti waitwe tena kwa ajili ya kuadhibiwa upya na kupewa nafasi ya kufika mbele ya Mahakama Kuu na ya kujitetea (mitigation) kabla ya kupewa adhabu mpya.

Katika hukumu yake iliyosomwa na Jaji Munisi jana imesema kifungu hicho alichokuwa akikipinga Kambole hakikinzani na katiba.

Jaji Munisi amesema kuwa suala hilo lilikwishaamuriwa na Mahakama ya Rufani na kuweka msimamo katika suala la adhabu ya kifo.

Amesema kanuni za kisheria za kufuata maamuzi, uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani unawafunga wao majaji wa Mahakama Kuu.

Akizungumzia hukumu hiyo, wakili aliyekuwa akimwakilisha Kambole katika kesi hiyo, Fulgence Massawe kutoka LHRC, amelieleza Mwananchi leo Ijumaa Julai, 19,2019 kuwa jambo zuri katika hukumu  ni kuwa mahakama hiyo imetoa nafasi kwa upande ambao haukuridhia kuomba mapitio ya hukumu hiyo Mahakama ya rufani.

“Kwa hiyo kwa sasa tunafuatilia nakala ya hukumu kwa ajili ya kufanya mchakato mwingine wa hatua zaidi za kisheria,” amesema Massawe.

Kwa mujibu wa hati ya  madai, kiapo  na hoja alizoziwasilisha mahakamani, Kambole alikuwa akidai kuwa masharti ya lazima ya adhabu ya kifo yanakinzana na Katiba kwa kukiuka haki ya kutokubaguliwa kama inavyotolewa katika Ibara ya 13 (1) ya katiba.

Amebainisha kuwa katiba ya mwaka 1977 na marekebisho yake, hutoa haki ya kuishi na haki ya ulinzi sawa chini ya sheria, lakini masharti ya kifungu hicho humnyima haki hizo mtu aliyetiwa hatiani kwa makosa hayo.

Amefafanua kuwa kifungu hicho huondoa usawa katika mashtaka kwani mtu aliyetiwa hatiani kwa kosa hilo haruhusiwi kujitetea dhidi ya adhabu, kama ilivyo kwa washtakiwa wa makosa mengine yasiyo ya mauaji, ambao hujitetea ili mahakama iwapunguzie adhabu.

Pia, alikuwa akidai kuwa mtu anapotiwa hatini kwa makosa ya mauaji naye ana haki kusikilizwa kwa usawa utetezi wake kuhusu kiwango cha adhabu na haki ya kukata rufaa dhidi ya hatia na adhabu anayopewa kama Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba inavyoelekeza.

Kambole ambaye alijitambulisha kama raia wa Tanzania mzalendo mwenye kutambua haki za binadamu, alikuwa anadai kuwa mazingira yanayosababisha makosa ya mauaji hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine au tukio moja na jingine.

Alikuwa akidai kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya uchaguzi wa kutoa adhabu kulingana na mazingira ya kesi, lakini kifungu hicho kinaiondolea haki yake ya uchambuzi sahihi na tathmini kabla ya kutoa adhabu.