Makonda awapigia debe wazawa

Wednesday May 01 2019
pic makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaeleza wataalamu wa mkoa huo kuwa hataki kuona kila  wakati miradi mikubwa wakipewa wageni huku wazawa wakiwekwa pembeni.

Makonda amesema hayo jana Jumanne wakati akizungumza na watendaji mbalimbali wa mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema utaratibu wa kila mradi mkubwa kupewa wakandarasi wa kigeni hauwezi kuwasaidia na kuwainua wakandarasi wazawa.

“Haya makampuni ya wazawa yatakuwa lini? Lazima tuweke sheria itakayoeleza asilimia 40 itafanywa na wazawa. Sasa hivi mkiandika mapendekezo mnatafuta kampuni yenye uzoefu mkubwa wa Sh 30 bilioni itatoka wapi wakati kazi mnazowapa  zinaanzia  Sh 200 milioni hadi 300 milioni.”

“Kwa taarifa yenu hata hizo kazi kampuni kubwa mnazowapa hawafanyi wao. Kuna kampuni moja sitaki kuitaja imechukua kazi kubwa lakini imetafuta kampuni  ndogo imekiunganisha itekeleze mradi huo na mwisho wa siku inajitengenezea jina yenyewe,” alisema.

Makonda amesema hatua hiyo inasababisha kampuni  za wazawa kuendelea kulalamika hali ngumu, huku jambo hilo likichangiwa na wataalamu.

Advertisement

Mkuu huyo wa mkoa alisema Rais John Magufuli ameelekeza miradi lazima ijenge hali ya uchumi ya wananchi, lakini kuna mradi mmoja wa Sh 70 bilioni unaotarajiwa kuchukuliwa na Mchina alienda kufanya kazi Dodoma kwa kutumia kampuni nyingine aliyoipa gawio.

“Sasa hivi  Mchina huyu anaitwa ana uzoefu kwa sababu alienda kufanya kazi Dodoma na anakuja kupewa mradi  Dar es Salaam.Wamejengeana uwezo wao, mimi sina ugomvi na Wachina au wawekezaji wa nchi za nje, lakini  ugomvi wangu ni kuhakikisha mzawa anapata kazi,” amesema Makonda.

Mmoja wa wanachama wa Chama cha Wakandarasi Wazalendo (ACCT), Clements Sanga alisema alichokisema Makonda ni sahihi na ndicho kilio kikubwa cha chama hicho kwa muda mrefu.

“Nchi za wenzetu kila mradi unapotekelezwa kunakuwa na ushirikishaji kikamilifu wa wakandarasi wazawa. Kinachotakiwa tushirikishwe ili hawa wageni wakiondoka wakandarasi wazawa wanatuaachia teknolojia na ujuzi utakaosaidia kwenye utekelezaji wa  miradi mingine,” amesema Sanga.

Advertisement