Mawakili walivyopambana rufaa ya dhamana ya Mbowe, Matiko

Machi 7, mwaka huu, ilikuwa siku ya furaha kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Esther Matiko, baada ya Mahakama Kuu Dar es Salaam kuwaachia huru kutoka mahabusu.

Mbowe, mbunge wa Hai na Matiko, mbunge wa Tarime mjini, walikaa mahabusu katika gereza la Segerea kwa siku 104 baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwani hadi wanarejea uraiani, mawakili wao walipambana vikali kwa hoja za kisheria, kwanza kwa kushinda pingamizi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), rufaa ya DPP, Mahakama ya Rufani hatimaye kushinda rufaa yao Mahakama Kuu.

Makala haya yanaangazia majibizano ya mwisho ya kihoja wakati wa usikilizwaji wa rufaa yao Mahakama Kuu ambayo yaliwapa hatima hiyo.

Usikilizwaji wa rufaa

Siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo Machi 6, mawakili wa wabunge hao, Peter Kibatala na Jeremiha Mtobesya walitumia hoja mbili za rufaa kujenga hoja kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu.

Katika hoja ya kwanza wakili Kibatala alidai kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kuwafutia dhamana kwa sababu za kutokufika mahakamani wakati wadhamini wao walikuwepo.

Alidai kuwa siku ambazo warufani hawakuwepo mahakamani, wadhamini wao walieleza sababu za kutofika kwao na hata siku waliyofutiwa dhamana, walikuwepo mahakamani.

Hivyo, alidai haikuwa sahihi katika mazingira hayo kwani hapakuwa na sababu za msingia kuwafutia dhamana, bali mahakama ya Kisutu katika uamuzi wake ilizizingatia taarifa za kiapo cha mmoja wa mawakili wa Serikali, walioendesha kesi hiyo, jambo alilosema si sahihi.

Wakili Kibatala alisisitiza kuwa hata kiapo hicho hakikuwasilishwa mahakamani kwa misingi ya kisheria na wao hawakupata nafasi ya kukijibu, licha ya kuomba nafasi hiyo, hivyo hakimu kwa kuzingatia taarifa za kiapo hicho, alitoa uamuzi wa upande mmoja.

Katika hoja ya pili wakili Mtobesya alidai kuwa mahakama ya Kisutu ilikosea kuwafutia dhamana warufani hao bila ya kuwapa wadhamini wao fursa ya kujieleza kwa nini mafungu yao ya dhamana yasitwaliwe.

“Katika kesi hii wadhamini walikuwepo cha kushangaza dhamana ilifutwa bila wao kutakiwa kusema chochote kuhusu dhamana hiyo,” alidai wakili Mtobesya.

Mawakili wa Serikali wajibu mapigo

Wakijibu hoja hizo, jopo la mawakili watano wa Serikali likiongozwa na mawakili wakuu, Faraja Nchimbi na Paul Kadushi walidai kuwa hoja za warufani hao hazina msingi kisheria, huku nao wakirejea kesi mbalimbali.

Wakili Jackline Nyantori alidai kuwa warufani hao kufutiwa kwao dhamana kulitokana na mwenendo wa washtakiwa kushindwa kufika mahakamani kwa nyakati tofauti na kwamba kabla ya hapo walikuwa wameshaonywa mara kadhaa.

Huku akitaja tarehe ambazo warufani hao hawakuwepo mahakamani na ambazo mahakama ilikuwa imeshawapa maonyo, alidai kuwa tabia hiyo ililenga kuchelewesha usikilizwaji wa kesi kwa maksudi na kwamba mahakama ina mamlaka kudhibiti mwenendo wa mashauri yake.

Alidai washtakiwa kuwepo mahakamani siku waliyofutiwa dhamana na kabla ya kukamtwa si sababu ya mahakama kutokuchukua hatua kwani ilishatolewa amri ya kuwakamata ili wajieleze ni kwa nini wasifutiwe dhamana kwa makosa hayo.

Alisisitiza kuwa kabla ya kuwafutia dhamana walipewa nafasi ya kujieleza wao na wadhamini wao na mahakama ilipima maelezo yao ikaona hayana msingi, yanajikanganya.

Wakili Nyantori alidai kuwa mdhamini na mshtakiwa kila mmoja ana wajibu na kuwajibika kwa kosa lake, huku akidai matokeo ya mdhamini kushindwa kumfikisha mahakamani mshtakiwa ni tofauti na mshtakiwa mwenyewe kutofika mahakamani.

Alidai kuwa hata kama mahakama ingetwaa mafungu ya dhamana ya wadhamini isingeondoa matokeo ya washtakiwa kufutiwa dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana.

“Kila mmoja anabeba msalaba wake na hawa wanabeba msalaba wao kwa kutofika mahakamani na hii haina uhusiano na wadhamini. Uvunjaji wa masharti ya dhamana unaondoa haki ya dhamana kisheria,” alisisitiza.

Mawakili wa Serikali, Salum Msemo na Nchimbi waliisisitiza kuwa Mahakama ya Kisutu katika uamuzi wake haikuzingatia taarifa za viapo walivyovilalamikia bali maelezo ya utetezi wa mkanganyiko wa washtakiwa. Hata hivyo, walidai kuwa mawakili wa warufani hawakuvipinga wala hawakuomba nafasi ya kuwasilisha viapo kinzani badala yake walivijibu kwa mdomo, jambo linalodhihirisha kuwa waliridhika navyo. Waliiomba mahakama iitupilie mbali rufaa hiyo.