Mchuano wa Lissu ndani, nje ya nchi

Muktasari:

Mbunge wa Geita (CCM),  Joseph Kasheku 'Musukuma' amehoji ni lini Bunge litasitisha mshahara wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),  Tundu Lissu aliyedai kuwa amepona na sasa anaitukana Serikali

Dar/Dodoma. Mapambano ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu dhidi ya Serikali yamezidi kushika kasi baada ya juzi kuvaana na balozi wa Tanzania nchini Marekani, huku Bunge likiibukiwa na mjadala kuhusu stahiki zake.

Wiki iliyopita, balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Posi alilazimika kujibu kwa taarifa ya karatasi mbili tuhuma mbalimbali zilizotolewa na mnadhimu huyo wa kambi ya upinzani kuhusu mazingira ya kushambuliwa kwake na jinsi anavyoona kuwa Jeshi la Polisi halijachukua hatua ipasavyo kuwasaka waliomshambulia.

Na juzi ilikuwa zamu ya balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masingili. Waziri huyo wa zamani aliungana na Lissu katika kipindi cha Straight Talk Africa kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Sauti ya Marekani (VOA) kujibu tuhuma za mbunge huyo ambaye alishambuliwa kwa zaidi ya risaasi 30 Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya nyumba yake, Area D mjini Dodoma.

Mjini Dodoma, suala la Lissu liliibuka jana wakati mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku ‘Msukuma’, alipotaka mwongozo wa Spika kuhusu ziara za Lissu barani Ulaya na Marekani, akipendekeza mshahara wake usitishwe.

Lakini mapambano makubwa yalikuwa studio za VOA jijini Washington, Marekani juzi, ambako mjadala ulimuhusisha pia Jon Temin kutoka taasisi ya Freedom House na mwanasiasa wa upinzani wa Uganda, Robert Chagulani maarufu kama Bobi Wine aliyeshiriki kwa njia ya Skype kutoka Kampala, Uganda.

“Unaweza kutufafanulia. Katika hali kama hii, ndugu yako Tundu Lissu alikuwa hatarini kuuawa katika eneo lililo katikati ya mji mkuu Dodoma wakati wa mchana na dereva wake hakuguswa na risasi hata moja. Amesema na nimeona, hii ni sehemu ambayo inawekewa ulinzi kwa saa 24,” aliuliza muongozaji wa kipindi hicho, Shaka Ssali.

Akijibu swali hilo, Balozi Masilingi alisema licha ya eneo hilo kuwa na nyumba za Serikali, halina uhusiano na kubanwa kwa uhuru wa kujieleza.

“Huwezi kuhusisha hilo moja kwa moja na uhuru wa kujieleza bila kuweka uthibitisho. Ndugu yangu alishambuliwa. Rais alitoa tamko la kulaani tukio hilo na kutaka vyombo vya dola kuchunguza. Kila mtu aliguswa na tuko hilo,” alisema Balozi Masilingi.

“Uchunguzi bado unaendelea, wanamsubiri arudi atoe ushirikiano. Dereva wake anasubiriwa kutoa ushirikiano. Sasa utakuwaje jaji kuhukumu hilo?”

Hata hivyo, Lissu alipotakiwa kuchangia suala hilo, alipinga vikali hoja ya balozi na kuendelea kuhoji sababu za eneo hilo kuondolewa walinzi na vifaa vya ulinzi kabla ya shambulio.

“Nilishambuliwa kwenye nyumba za Serikali, nilipigwa mara 16 na nimefanyiwa operesheni 22. Swali la kujiuliza; nani aliyetoa agizo la kuondoa ulinzi katika nyumba za Serikali?” alihoji

“Pili, hilo eneo linalindwa na CCTV. Ziliondolewa siku moja kabla ya tukio. Hakuna anayejua zilikopelekwa kwa sababu polisi hawasemi. Ninazungumza na watu, hakuna mtu aliyehojiwa.”

Kuhusu uhuru wa kujieleza, Lissu alisema Tanzania imeingia katika janga la kutokuwa na uhuru wa kujieleza ikiwa pamoja na kufanya siasa, akihoji sababu ya sheria ya kosa la uchochezi kuendelea kuwepo.

“Tangu mwaka 1953 tunayo sheria ya uchochezi, Uchochezi ni kosa linalokwaza uhuru wa kujieleza. Sababu ya kutungwa mwaka 1953 ilikuwa ni utawala wa kikoloni ili kuwabana wazalendo waliokuwa wakidai uhuru,” alisema.

“Mtu wa kwanza kubanwa na sheria hiyo alikuwa Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa mwenyekiti wa Tanu na wengine wawili.”

Alisema ilitegemewa sheria hiyo ingeondolewa baada ya uhuru, lakini hilo halijafanyika na ndio maana anaendelea kukabiliwa na mashitaka ya uchochezi. Pia alisema suala la kuwa mbaroni kwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime, Esther Matiko ni sehemu ya kuwanyima raia haki zao.

Hata hivyo, Balozi Masilingi alisema uhuru wa kujieleza na kufanya siasa unatambuliwa na Katiba na sheria, lakini akasema Serikali haiwezi kuruhusu watu kutumia uhuru huo kuingilia uhuru wa wengine.

“Huwezi kuacha mtu aumize wengine, huwezi ukaacha mtu achafue wengine ashushe hadhi za wengine,” alisema.

Wawili hao pia walipambana katika suala la uchunguzi wa shambulizi la Dodoma, Lissu akiendelea kuhoji sababu za Jeshi la Polisi kutomfuata nje ya nchi kwa ajili ya kumuhoji na kulituhumu kutoanza upelelezi wala kukamata washukiwa, huku Masilingi akiendelea na msimamo wa Serikali kuwa mbunge huyo wa dereva wake wanasubiriwa Tanzania.

Suala hilo pia liliibuka Dodoma wakati wa kujadili taarifa ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, ambako mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alihoji sababu za Serikali kutotumia sheria zake kutuma watu kwenda kumuhoji Lissu.

Selasini alisema Sheria ya Upelelezi ya Masuala ya Kijinai inawezesha mtu kuchukuliwa maelezo popote.

“Lissu angefuatwa Nairobi, Ubeligiji, kwa kutumia sheria hiyo ambayo tuliitunga wenyewe hapa bungeni. Sasa tukitoa matamko ambayo watoto wetu watakuja kuyasoma kwenye Hansard (kumbukumbu rasmi za Bunge) kwa kufanya reference tunaonekana sijui sisi ni wabunge wa namna gani,” alisema.

Hata hivyo, Spika Job Ndugai alimkatisha, akisema wanamlaumu bure Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, akitoa mfano kwamba dereva wa Lissu anaweza kurudi nchini ili kutoa ushahidi.

Lakini Selasini alijibu kuwa Lissu na dereva wake bado wako kwenye matibabu na kwamba wanaoweza kutolea maelezo ya matibabu ni madaktari wanaowatibu. “Lakini hii sheria hii wizara ya Mambo ya Ndani inaweza kuitumia hata kwa huyu dereva popote alipo akahojiwa,” alisema.

Kauli hiyo iliibua swali jingine kutoka kwa Spika Ndugai akitaka kufahamu iwapo madaktari walishaandika chochote na kuleta nchini, lakini Selasini alijibu kuwa ili kuondoa sintofahamu na kelele zinazopigwa mitaani ni vyema sheria hiyo ikafuatwa.

Hata baada ya jibu hilo, Ndugai bado alimweleza Selasini kuwa madaktari wanapaswa kuandika taarifa ili ije nchini.

Jijini Washington, Balozi Masilingi pia alijibu hoja kuhusu kufutwa kwa dhamana ya Mbowe na Matiko, akisema wawili hao bado hawajafungwa bali wamekuwa rumande kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Hata hivyo, Ssali alimuuliza kama ni kweli mtu anayekuja Tanzania hawezi kutoa maoni kinyume na chama tawala, lakini Masilingi alisema ni uongo mtupu.

Wakati hayo yakiendelea, jana Bunge lilikuwa na mjadala kuhusu haki za Lissu baada ya Msukuma akiomba mwongozo.

“Lissu anazunguka huku anasomeka anaumwa. Ni lini Bunge litasitisha mshahara wake kwa sababu ameshapona na anaendelea kuzungukazunguka huko na huko akitukana Bunge na Serikali?” alihoji Msukuma.

Spika Job Ndugai alimjibu kuwa suala hilo linahitaji kuangaliwa kwa upekee kwa kuwa mbunge huyo hayupo jimboni, bungeni, hospitali wala nchini.

“Na mimi sina taarifa zake kabisa na wala hajishughulishi kuniandikia spika niko mahali fulani. Nafanya hivi na kama ni mgonjwa hakuna taarifa yeyote ya daktari. Halafu unaendelea kumlipa malipo mbalimbali,”alisema Spika huku baadhi ya wabunge wakipiga makofi.

Alisema anadhani hoja ya Msukuma ina msingi.

na kuwa ipo haja ya kusimamisha malipo mpaka hapo watakapopata taarifa za sehemu aliko na anafanya nini kwa kuwa hilo linaweza kuwa hoja ya ukaguzi

“Tulikuwa tunajua yuko hospitali, sasa tunamuona yuko duniani. Kwa maneno ya Msukuma anazurara. Nikuhakikishie yale yaliyo ndani ya uwezo wangu nitayafanya,” alisema.

Lakini mara moja, Chadema wakatoa taarifa kumpinga Spika wakitaja majini ya wabunge ambao wamewahi kuwa nje ya chombo hicho cha kutunga sheria kwa muda mrefu kwa ajili ya matibabu, akiwemo Ndugai.

“Chadema tunasikitishwa na kauli hizi kwani ni uthibitisho wa wazi kuwa Bunge lilipokataa kulipia matibabu ya Lissu walikuwa wana nia mbaya dhidi ya maisha yake na walipoona Watanzania wameendelea kulipia matibabu yake, imewaumiza,” inasema taarifa hiyo ya Chadema.

Chadema imemtaka Spika asimamie sheria na kanuni za Bunge na haki zilizopo kwa mujibu wa sheria kwa kuwa wabunge “hawafanyi kazi zao kwa kutegemea fadhila”.

Juzi jioni suala la Lissu liliibuka tena wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliposema kesi ya shambulio la Lissu imetelekezwa kwa mbunge huyo na dereva wake wameshindwa kutoa ushirikiano kwa polisi.

Akijibu hoja za wabunge kuhusu taarifa ya kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Lugola alisema: “Kesi ya Tundu lissu imetekelezwa. Gari lilikuwa na watu wawili baada ya tukio hilo key witness (mashuhuda muhimu) wamepotea katika mazingira ya kutatanisha,” alisema.

“Ingawa ameshapona, kwa nini harudi kuja kutusaidia. Sisi hatuwezi kujua ni wembamba au wanene. Aje ili atusaidie,” alisema.

Hata hivyo, wakati wote Lugola anaeleza wabunge wa upinzani waliomba kutoa taarifa bila mafanikio baada ya Naibu Spika Dk Tulia Ackson kusema kuwa

alishakataa taarifa wala muongozo tangu awali.