Mkurugenzi tukio la mauaji Itigi apandishwa kizimbani

Muktasari:

Mkurugenzi wa halmashauri ya Itigi, Pius Luhende (54) na washtakiwa wenzake sita leo Jumatatu Februari 11, 2019 wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoani Singida wakidaiwa kumuua, Isaka Petro.

Singida. Mkurugenzi wa halmashauri ya Itigi, Pius Luhende (54) na washtakiwa wengine sita  leo Jumatatu Februari 11, 2019 wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoani Singida wakikabiliwa na shtaka moja la mauaji ya Isaka Petro.

Washtakiwa wengine ni Rodney Elias, Makoye Stephen, Erick Paul ,Eliutha Augostino, Silivanus Lugwisha na Yusuf John (25).

Mwanasheria wa Serikali mkuu, Emil Kiria amedai mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Consolata Singano kuwa Februari 2, 2019 eneo la genge 48 kijiji cha Kazikazi kata ya Kitaraka tarafa ya Itigi, washitakiwa kwa pamoja walimuua Petro.

Kiria amesema washitakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na sheria kanuni ya adhabu kifungu cha 116 na 197.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Kiria amesema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutaja kesi hiyo.

Hakimu Singano amesema kwa vile kosa hilo halidhaminiki, washitakiwa wataendelea kuwa chini ya ulinzi hadi Februari 25, 2019 itakapotajwa tena.