VIDEO: Mwanasheria azungumzia kiongozi genge dawa za kulevya kufungwa maisha, kuongezewa miaka mingine 30

Muktasari:

Mwanasheria wa kujitegemea, Reuben Simwanza amesema hukumu ya kifungo cha maisha jela na nyongeza ya miaka mingine 30 alichopewa Joaqui Guzman maarufu El Chapo baada ya kutiwa hatiani na makosa 10, ni cha kawaida kwa mujibu wa sheria


Dar es Salaam. Mwanasheria wa kujitegemea, Reuben Simwanza amesema hukumu ya kifungo cha maisha jela na nyongeza ya miaka mingine 30 alichopewa Joaqui Guzman maarufu El Chapo baada ya kutiwa hatiani na makosa 10, ni cha kawaida kwa mujibu wa sheria.

Amesema hukumu hiyo si ya kwanza kutolewa kutokana na mazingira ya makosa aliyokutwa nayo.

Mbali na kifungo hicho kilichotolewa na Mahakama ya New York nchini Marekani juzi Jumanne Julai 16, 2019, El Chapo aliyewahi kutoroka gereza la Mexico mwaka 2015 kupitia shimo lililochimbwa kwenye chumba chake, ametakiwa kulipa Dola12.6 bilioni za Marekani.

Mbali na kusafirisha dawa za kulevya kosa lake jingine ni utakatishaji wa fedha.

Katika maelezo yake Semwanza amesema El Chapo alishtakiwa kwa makosa 10, ambayo kimsingi kupatikana kwa hatia kwa kosa moja, haizuii kupata adhabu kwa kosa jingine.

“Inapotokea umekutwa na hatia kwa kosa moja, hii haizuii kupata adhabu unapokutwa na kosa katika kesi nyingine,” amesema Simwanza akisema hicho ndicho kilichookewa kwa El Chapo.

Guzman alikuwa kiongozi wa kundi la Sinaloa Cartel lililokuwa maarufu kwa kuua, kuteka, kutakatisha fedha na kusafirisha dawa za kulevya nchini Marekani lililoanzishwa mwaka 1989.

Mwaka 2015 alitoroka gerezani kupitia shimo lililochimbwa chumbani kwake  ila alikamatwa  mwaka 2017 na kupelekwa Marekani.