Nandy: Nilisikia mengi mabaya kuhusu Ruge lakini nilimpenda hivyo hivyo

Tuesday May 14 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Hakika Nandy alikolea kwa marehemu Ruge Mutahaba. Hivi ndivyo tunavyoweza kusema maana kwa hadithi hii tamu ya mapenzi hakuna maneno mengine yanaweza kutumika.
Nandy ameeleza kwa kina kuhusu uhusiano huo uliodumu kwa muda wa miaka mitatu na ukatenganishwa na kifo mwezi mmoja kabla ya ndoa yao.
Msanii huyu ameeleza kuwa awali alipata wakati mgumu kumkubali Ruge kutokana na aliyokuwa akiyasikia kumhusu lakini taratibu akamuelewa na kumuona kuwa ni mtu sahihi kwake.
“Alikuwa ananitumia meseji nikawa nafanya kama sizioni, ikapita muda kuna siku akaamua kuniita sehemu ili tuzungumze uso kwa uso nikamsikiliza na huo ndiyo ukawa mwanzo wa ukaribu wetu kama wapenzi,” amesema Nandy alipozungumza na Millard Ayo jana Aprili 13.
Amesema licha ya kuwa walikuwa walipendana sana kuna wakati walipishana lakini ugomvi wao haukuwahi kudumu kwa zaidi ya saa tatu bila kupatana.
“Ilikuwa inatokea tunapishana ila hatujawahi kuwa kwenye ugomvi kwa zaidi ya saa tatu bila kupatana na chanzo kikubwa cha ugomvi inakuwa kutopokea simu na mara nyingi tatizo hilo linakuwa kwangu,”
Amesema uhusiano wake na Ruge ulikuwa bora kuliko mahusiano mengine yote aliyowahi kupita na pengo la mwanamume ni kubwa mno kwake.
 “Namkumbuka kwa mengi alikuwa ni mtu anayejua na kufuatilia vitu vingi, yaani hata mawazo yangu mtu wa kwanza kumwambia ni yeye hata kama ni pumba ananisikiliza hadi mwisho halafu ananishauri, nikiwa na huzuni namfuata yeye hata umbea namwambia lakini sasa hivi kuna wakati nakutana na vitu natamani nimwambie ila ndio nashindwa.”
Akizungumzia kilichomvutia Ruge kwake amesema ni tabia yake ya kwenda kanisani na kujiweka karibu na Mungu.
Amesema Ruge alikuwa akivutiwa na namna Nandy anavyomtanguliza Mungu mbele katika maisha yake na wakati mwingine alikuwa akimkumbusha kwenda kanisani.
“Yaani hata kama yeye haendi kanisani alikuwa anafurahi kuniona mimi nikienda na wakati mwingine hata kunikumbusha, kuna muda nilikuwa nasali naye pamoja, namuombea hata kumletea maji ya baraka yaliyoombewa.”
“Pia, uchapakazi wangu ulikuwa ukimvutia sana nadhani hivyo vitu ndivyo vilimfanya anipende wakati mimi kwake nilipenda jinsi alivyoweza kuongoza maisha yangu, kunisimamia nitimize ndoto zangu na alikuwa mkweli mno.

Advertisement