Nandy: Ruge alifariki mwezi mmoja kabla ya ndoa yetu

Muktasari:

Walijiandaa kuwa na familia ya watoto wawili

Ikiwa ni takribani miezi mitatu sasa tangu tasnia ya habari impoteze mmoja wa wadau wa kubwa, Ruge Mutahaba, aliyekuwa mpenzi wake, mwanamuziki amemkumbuka kwa namna yake akieleza jinsi kifo  kilivyozima  ndoto zao.

Msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye jina lake halisi ni Faustina Charles, ameweka wazi kuhusu uhusiano wake na nguli hiyo ambaye enzi za uhai wake alikuwa Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group na kueleza kuwa walipanga kufunga ndoa Machi mwaka huu.

Jana akihojiwa na Millard Ayo, Nandy ameeleza uhusiano wao ulikuwa wa siri kwa kuwa walikubaliana kulifanya suala hilo kuwa binafsi mpaka watakapokamilisha taratibu zote.

Amesema kuwa mara kadhaa alikuwa akikanusha kuhusu uhusiano huo kwa kuwa waliona hakuna haja ya kuweka wazi.

“Hatukupenda uhusiano wetu uendeshwe na mitandao, tulikuwa tunajaribu kutengeneza njia ya maisha yetu binafsi ili kufikia lengo letu. Hatukutaka life style  (mtindo wa maisha) ya mahusiano ya awali ya Ruge yajitokeze kwenye maisha yetu,”

Nandy ameeleza kuwa uhusiano wao ulianza baada ya yeye kuanza kumshirikisha Ruge katika vitu vingi na na kwamba hata familia zao zote zilikuwa zikifahamu.

Kuhusu familia Nandy ameeleza kuwa tayari walipanga na mwenza wake kuwa na watoto pacha pale watakapoingia kwenye ndoa.

 

Ruge alifariki Februari 26, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.