Pacha walioungana kifuani wafariki wakipishana dakika

Muktasari:

  • Muuguzi huyo alisema baada ya vifo hivyo gari lililowapeleka lililazimika kumrudisha mama na miili ya watoto hao Geita kwa ajili ya taratibu za maziko ambapo ndugu walikabidhiwa.

Geita. Watoto pacha wawili kati ya watatu waliozaliwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita wamefariki dunia wakiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa uchunguzi.

Pacha hao na mwenzao walizaliwa Machi 17.

Watoto hao wawili waliokuwa wameungana katika eneo la kifua walipoteza maisha kwa nyakati tofauti kwani mmoja alifariki dunia wakati wakivuka kivuko cha Busisi wilayani Sengerema, huku mwingine akipoteza maisha mara tu baada ya kufika kwenye lango la hospitali hiyo.

Muuguzi mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Geita, Charugamba Jackson alisema jana kuwa, kwa mujibu wa muuguzi aliyekuwa akiwapeleka watoto hao Bugando, mtoto wa kwanza hali ilibadilika wakiwa kwenye kivuko na mapigo ya moyo kuanza kushuka.

“Wakiwa njiani muuguzi aligundua hali ya mtoto mmoja imebadilika na mapigo yake yalianza kushuka na anapumua kwa shida, alijitahidi kumsaidia lakini alifariki walipovuka,” alisema Charugamba.

“Alimtaka dereva kuongeza mwendo wa gari, lakini kwa bahati mbaya walipofika getini mtoto mwingine naye alifariki.”

Muuguzi huyo alisema baada ya vifo hivyo gari lililowapeleka lililazimika kumrudisha mama na miili ya watoto hao Geita kwa ajili ya taratibu za maziko ambapo ndugu walikabidhiwa.

Alisema mama wa watoto hao amelazwa katika hospitali hiyo huku mtoto mwingine aliyezaliwa wa kwanza akiendelea vizuri.

Alisema hospitali hiyo iliwapa rufaa watoto hao ili wakafanyiwe uchunguzi zaidi Bugando, lakini jambo hilo halikufanikiwa.

“Hatujajua walipishana muda gani kwa kuwa alivyofariki wa kwanza muuguzi alijitahidi kuendelea kumpa hewa mwingine na hakurekodi muda, tunahisi kuna walichokuwa wanategemeana kwa kuwa alivyobadilika aliyetangulia hata aliyefuata alibadilika hivyo hivyo na kufariki,” alisema.

Charugamba alisema mama wa watoto hao alipokewa hospitali hapo kutoka wilayani Nyang’hwale akiwa na matatizo ya upungufu wa damu na uchungu pingamizi.

Alisema walimsaidia na kujifungua mtoto wa kwanza bila shida, lakini baada ya uchunguzi ilibainika bado ana mtoto tumboni.

Alisema kutokana na mtoto mwingine kutanguliza mkono ililazimu mama huyo kufanyiwa upasuaji uliosaidia kuwatoa watoto walioungana wakiwa wazima, lakini waliamua kuwapeleka Bugando kwa uchunguzi wa madaktari bingwa.

“Hatukuona kama ni busara kumpa rufaa ya haraka haraka, hivyo tulikaa na mama kwa saa 24 ili tuone anavyoendelea, na alivyoonekana afya imetengemaa ndipo tuliwapa rufaa kwenda Bugando.”

Mwananchi lilipotaka kuonana na mama wa pacha hao hospitalini hapo, muuguzi huyo alisema kwa sasa hayuko tayari kutokana na taarifa za awali kupokewa kwa mtazamo tofauti na jamii.