Profesa Assad afunguka

Dar es Salaam. Hatimaye Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amefunguka kuhusu baadhi ya tuhuma dhidi yake kuwa alilidharau Bunge baada ya kutumia neno “udhaifu” katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Profesa Assad amesema anashutumiwa bila ya makosa na kwamba anaichukulia hatua hiyo ya Bunge kwa utulivu na suala hilo halimsumbui.

Bunge lilifikia azimio la kutoshirikiana na Profesa Assad mapema wiki hii baada ya kumkuta na hatia ya kusema “udhaifu wa Bunge” wakati alipohojiwa kuhusu kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake ambazo huibua ufisadi, kutofuatwa kwa kanuni za fedha, kasoro zinazosababisha kuwepo na wafanyakazi hewa na nyingine za kiutendaji.

CAG Assad, ambaye kwa kawaida si mzungumzaji wa mara kwa mara na vyombo vya habari, jana alikubali kutoa muda wake kuzungumzia sakata hilo.

Aliiambia gazeti la The Citizen linalochapishwa na Mwananchi Communications Limited (MCL), kuwa hajui sababu zilizosababisha Bunge lifikie uamuzi wa kutoshirikiana naye, akisema anadhani hakufanya kosa. “Kumekuwa na tuhuma kwamba niliita Bunge kuwa ni dhaifu, lakini hizo hazina msingi,” alisema Profesa Assad katika mahojiano maalumu.

Kama ambavyo amekuwa akisema kabla ya kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili, Hadhi na Haki za Bunge, Profesa Assad, ambaye aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2014, alisema matumizi ya neno “udhaifu” katika lugha ya ukaguzi ni la kawaida na kwamba si yeye aliyeliunda.

Alisema limekuwa likitumiwa mara kwa mara katika nyaraka rasmi, ikiwa ni pamoja na taarifa za ukaguzi wa hesabu za Serikali.

Hoja ya kutaka Bunge liliridhie mapendekezo ya kamati ya kutoshirikiana na Profesa Assad haikupita bila ya kupingwa ndani ya Bunge, ambalo limetawaliwa na CCM.

Wabunge wa upinzani walilipinga suala hilo na kuonya kuwa linaweza kusababisha mgogoro wa kikatiba na mmoja wao, Godbless Lema aliungana na Profesa Assad kusisitiza kuwa Bunge ni dhaifu, hali iliyosababisha naye apelekwe mbele ya kamati hiyo.

Wabunge hao walitoka ndani ya ukumbi wakati Naibu Spika, Tulia Ackson alipoamuru Lema atoke.

Baadaye, Lema aliadhibiwa kwa kutakiwa asihudhurie mikutano mitatu ya Bunge, akiwa ni wa pili katika sakata hilo baada ya mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuzuiwa kuhudhuria mikutano miwili kutokana na kuungana na kauli ya Profesa Assad wakati akihutubia mkutano wa hadhara.

Jana, alipoulizwa tuhuma kuwa alitoa maneno hayo dhidi ya Bunge wakati akiwa nje ya nchi, Profesa Assad alisema si sahihi.

“Nilifanya mahojiano hayo wakati nilipotembelea Umoja wa Mataifa, ambao Tanzania ni mwanachama,” alisema.

“Nikiwa Umoja wa Mataifa, nilihojiwa na idhaa ya Kiswahili na mwandishi wa habari Mtanzania ambaye aliibua masuala yanayoihusu Tanzania. Kwa hiyo haitakuwa sahihi kusema nilikuwa nazungumzia mambo ya ndani nikiwa katika ardhi ya nje.”

CAG alirudia kauli yake kuwa hafikirii kujiuzulu nafasi yake, akisema ataendelea na kazi yake kama kawaida.

Hatua ya Bunge kusema halitashirikiana naye imeibua wakosoaji, ambao wengi wanamuunga mkono Profesa Assad, ikiwa ni pamoja na wanasiasa, wanasheria, taasisi za kijamii huku mjadala mkubwa ukiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Wengi wanaonyesha kushangazwa na uamuzi huo, hasa baada ya Spika Job Ndugai kufafanua kuwa walichoamua ni kutofanya kazi na Profesa Assad na si ofisi ya CAG, huku wakosoaji wakisema haiwezekani kutofautisha ofisi ya CAG na mkuu wake.

Wanasema hata ripoti, ambayo inatakiwa iwasilishwe bungeni siku saba za mwanzo za Bunge la Bajeti, imetiwa saini na Profesa Assad, kitu kinachoonyesha haitawezekana kumtenga na kazi yake.

Mtangulizi wake, Ludovick Utouh wa taasisi ya Wajibu, ambayo inafanya harakazi za uongozi bora, ni kati ya watu walioshtushwa na uamuzi huo wa Bunge, akionya kuwa unaweza kusababisha mgogoro baadaye.