Sababu kupanda kwa pato la kila Mtanzania

Muktasari:

Serikali imeeleza sababu za kupanda kwa kipato cha kila Mtanzania kwa zaidi ya Sh100,000 mwaka 2018. Kulitokana na kukua kwa pato la Taifa kulikochangiwa na sababu kadhaa.

Dar es Salaam. Hali nzuri ya hewa iliyochangia uzalishaji wa chakula na mazao mengine ya kilimo pamoja na kuimarika kwa huduma za usafirishaji, Serikali imesema zilikuwa sababu za kuimarika kwa kipato cha kila Mtanzania mwaka jana.

Sababu nyingine, imesema ni kuongezeka kwa uwekezaji katika miundombinu ya barabara, reli, na viwanja vya ndege pamoja na upatikanaji wa umeme.

Shughuli zilizokua kwa kasi kubwa ni sanaa na burudani kwa asilimia 13.7, ujenzi asilimia 12.9, uchukuzi na uhifadhi mizigo asilimia 11.8, shughuli za kitaaluma, sayansi na ufundi asilimia 9.9, na habari na mawasiliano asilimia 9.1.

Licha ya sekta ya kilimo kukua kwa asilimia 5.3, ndiyo iliyongoza kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa ikichangia asilimia 28.2 na kufuatiwa na sekta ya ujenzi kwa asilimia 13 na biashara na matengenezo asilimia 9.1.

Mwaka 2018, Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilifanya maboresho ya takwimu za Pato la Taifa kwa kutumia mwaka 2015 kama mwaka wa kizio kutoka mwaka wa kizio wa 2007.

Kufuatia maboresho hayo, mabadiliko kadhaa yalijitokeza ikiwa ni pamoja na mfumo na ukubwa wa Pato la Taifa; viwango vya ukuaji  wa Pato la Taifa kisekta; mchango wa sekta mbalimbali katika Pato la Taifa; na uwiano wa viashiria mbalimbali kwa Pato la Taifa.

Kutokana na mwenendo huo, pato la Taifa lilikua kwa asilimia saba na kufika Sh129.4 trilioni mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.8 za mwaka 2017 iliofikisha Sh118.7 trilioni za pato la Taifa kwa bei za mwaka husika.

Aidha, mwaka 2018, Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu 52,619,314 ambao wastani wa pato la kila mmoja lilifika Sh2.458 milioni kutoka Sh2.327 mwaka 2017 sawa na ongezeko la Sh131,000.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa anawasilisha hali ya uchumi wa Taifa na kufafanua kwamba wastani wa pato la kila mtu kwa mwaka 2018 ni sawa na Dola 1,090 za Marekani zikilinganishwa na Dola 1,044 mwaka 2017.