Sababu za kuwalipa wakulima wa korosho bei pungufu ya Rais zatajwa

Tuesday February 5 2019

 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Baada ya kuwapo kwa malalamiko kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho, Serikali imetoa sababu za kuwalipa chini ya Sh3,300 iliyoagizwa na Rais.

Novemba mwaka jana, Rais John Magufuli aliutangazia umma kuwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko itanunua korosho zote za wakulima kwa Sh3,300 kwa kila kilo moja baada ya kampuni zilizopewa kibali cha kununua zao hilo kugomea bei.

Tangu agizo hilo lilipotolewa, kumekuwa na malalamiko kuwa wakulima wanapunjwa malipo ya korosho hivyo kuilazimu Serikali kufafanua kinachoendelea katika mikoa ya Kusini inayoongoza kwa kilimo cha zao hilo.

“Daraja la kwanza tunalipa Sh3,300 na daraja la pili Sh2,640 lakini korosho chafu tunawaambia wakasafishe na wakishindwa hatulipi kabisa,” alisema Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba bungeni jana. Alisema tamko la Rais lilitoa bei elekezi kwa korosho za daraja la kwanza na sio zote.

Alisema mpaka Januari 30, jumla ya tani 214,269.684 za korosho ghafi zenye thamani ya zaidi ya Sh707 bilioni sawa na asilimia 89.3 ya lengo la uzalishaji, zilikuwa zimenunuliwa na zaidi ya Sh424.84 bilioni kuingizwa kwenye akaunti za wakulima.

Kiasi kilicholipwa, alisema kilitokana na tani 134,535.904 za wakulima 390,466 kutoka vyama 603 vya msingi kati ya 605 vilivyohakikiwa.

Advertisement

Mgumba alitoa ufafanuzi huo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Cecil Mwambe (Chedema) aliyetaka kujua sababu za kuwalipa wakulima chini ya Sh3,300 kama ilivyoelekezwa na Rais Magufuli.

Mwambe alisema kuna ukiukwaji wa haki katika malipo ya korosho kwani wengi wanalipwa chini ya kiwango kilichotajwa huku wengine wakisumbuliwa.

Hakuwa Mwambe pekee aliyelizungumzia suala hilo, awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alitaka kujua kiasi cha fedha kilichotumika kufanikisha malipo ya wakulima hao na zilikotoka.

“Je, wakulima au vyama vya msingi vingapi vimelipwa na vingapi bado lakini zoezi zima linatarajiwa kuisha lini,” alihoji Mdee.

Katika majibu yake, naibu waziri Mgumba alisema “Operesheni korosho inakwenda vizuri na inatarajia kukamilika Februari 15,”

Hivi karibuni Serikali ilisema imeuza tani 100,000 za korosho kwa Sh4,180 kwa kila kilo moja kwa kampuni kutoka nchini Kenya ijulikanayo kama Indo Power.


Advertisement