TRA yafafanua mabango kwenye magari kudaiwa kodi

Dar es Salaam. Baada ya kusambaa kwa barua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikimtaka mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya International Tanfeed Limited kulipia Sh1.8 milioni za kodi ya tangazo katika gari la kampuni hiyo, mamlaka hiyo imefafanua juu ya kodi hiyo.

“Kuna mabango ya kawaida yamesimikwa, mabango yaliyo juu ya majengo na mabango ya kwenye magari ambayo gari kila likizunguka linakuwa na bango hilo, mfano kampuni za vinywaji, biashara ya bidhaa mbalimbali,” alisema mkurugenzi wa elimu kwa mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo.

“Sio kodi mpya na si kitu cha ajabu, magari haya yanastahili kulipiwa. Kwa mfano, bango lipo katika gari linazunguka nchi nzima linaonwa na watu wengi zaidi kuliko bango likiwekwa sehemu moja.”

Alisema matangazo yote yakiwamo yaliyo kwenye magari mbalimbali yanatakiwa kulipiwa ada ya mwaka kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017.

Katika barua hiyo ya Novemba 26, mwaka jana, meneja wa TRA mkoa wa kikodi wa Kinondoni alimtaka mkurugenzi wa kampuni hiyo kulipa kodi ya Sh1.8 milioni kwa matangazo yaliyomo katika gari hilo kwa mujibu wa sheria kupitia mfumo wa ukusanyaji mapato wa TRA kupitia namba GFS Code 14220177.

“Zingatia kwamba ikitokea umeshindwa kulipa kama ilivyobainishwa hapa (kwenye barua), mamlaka itatafuta namna ya fidia kiasi hicho dhidi yako kama ilivyobainishwa katika Sheria ya Kodi,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Katika ufafanuzi wake Kayombo alibainisha viwango vya tozo za matangazo ya mabango yaliyopo kwenye magari kuwa ni Sh10,000 kwa futi moja ya mraba.

Alisema tozo za matangazo mengine ya mabango yasiyowaka ni Sh10,000 kwa futi moja ya mraba, Sh13,000 kwa matangazo ya mabango yanayowaka kwa futi moja ya mraba na matangazo ya mpito (transition adverts) kwa kila futi moja ya mraba.

Awali, kodi za matangazo ya mabango zilikuwa zikikusanywa na Serikali za Mitaa lakini baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017, kodi hizo sasa zinakusanywa na TRA.

Akielezea zaidi kuhusu kodi hiyo Kayombo alisema, “Ipo kwenye sheria na si jambo geni lilikuwepo kabla hata kodi ya mabango haijahamishiwa TRA kutoka katika manispaa, kilichobadilika ni kuhamishiwa kwetu tu.”

“ Tangu 2017, TRA tunakusanya na kwa kweli siwezi kukumbuka tumekusanya kiasi gani maana takwimu hizo lazima nizikusanye.”

Pamoja na Kayombo kusema kwamba kodi hiyo si jambo jipya, baadhi ya wadau walisema hawajui lolote kuhusu matangazo hayo.

“Mpaka sasa sijui chochote kuhusu tozo hizo, wewe ndiyo kwanza unaniambia. Magari yetu yako kazini yakiwa na matangazo na hatujaletewa taarifa yoyote ya kututaka kulipia,” alisema meneja wa kampuni moja ya vyakula ambaye hakutaka kutaja jina lake.