Tamko la Taasisi ya Wajibu kuhusu sakata la Spika Ndugai, CAG

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa leo Jumatano na Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Wajibu imesema njia sahihi ya kumaliza sintofahamu iliyopo baina ya Spika wa Bunge, JOb Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad

Dar es Salaam. Taasisi ya Wajibu imesema busara inahitajika kutumika ili kumaliza sintofahamu iliyopo kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo ambayo imetoa taarifa kwa umma leo Jumatano Januari 9, 2019 ikielezea  suala hilo ikisema taasisi ya Wajibu imeona ni vizuri itoe maoni huru kwa kuzingatia maslahi mapana katika uwajibikaji na utawala bora nchini.

“Ifahamike Bunge na CAG ni vyombo vinavyotambulika na kulindwa Kikatiba,” inaeleza taarifa hiyo ya Bodi  ambayo mkurugenzi wake ni Ludovick Utouh aliyewahi kuwa CAG

“Kwa kuzingatia umuhimu wa taasisi hizi mbili katika kusimamia rasilimali za umma na kukuza uwajibikaji na utawala bora, ni vyema busara ya hali ya juu itumike baina ya pande hizi mbili katika kutatua mgogoro huu kwa sababu dhana ya uwajibikaji na utawala bora nchini itaimarika iwapo tu kutakuwepo na uhusiano mzuri kati ya taasisi zote za uwajibikaji na usimamizi nchini,”  imeongeza

 

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa kutokana na umuhimu wa taasisi hizi mbili ambazo zinatakiwa kushirikiana kwa karibu sana katika kuimarisha uwajibikaji na utawala bora hapa nchini, wananchi wanashauriwa kutoa maoni yatakayoboresha na kuimarisha uhusiano wa taasisi hizi.

“Kwa muktadha huo, Wajibu inaamini kwamba sintofahamu iliyojitokeza kati ya CAG na Bunge ni vyema ikashughulikiwa kwa busara kati ya pande zote mbili bila kuathiri uhuru wa kikatiba uliotolewa kwa mhimili wa Bunge na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,” imeeleza