Wafanyabiashara wa nafaka soko kuu Mtwara kimbunga hakija watisha

Mtwara. Baadhi ya wafanyabiashara wa nafaka kama mchele na maharage katika soko kuu la Mtwara wanaendelea na biashara zao kama kawaida lakini wauzaji wa mbogamboga na bidhaa nyingine wamefunga biashara zao kujihadhari.

Pia wafanyabiashara ambao fremu za biashara zinazunguka soko hilo baadhi yao wamefungua milango nusu na kuendelea kuuza bidhaa kwa wateja wanaofika kuhitaji huduma.

Baadhi ya wafanyabiashara wa nafaka wamesema wanaendelea na biashara kwani wana amini tukio hilo litakuwa la kheri na Mungu atawaepusha.

“Kama kina kheri nasi (kimbunga) sawa na kama kina shari Allah atuepushie,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Mfanyabiashara mwingine amesema: “Wengine toka tumezaliwa tumewahi kukiona kimbunga na kama leo wote tukifunga nani atahudumia wengine?” amehoji.

 Baadhi ya wateja wa nafaka wameonekana wakiendelea kufanya manunuzi kama kawaida, huku moja ya maduka ya vinywaji mbalimbali katika eneo la Umoja likiwa limefunguliwa huku baadhi ya watu wakiwa wamekaa nje.