Watumishi 183 ardhi wanaodaiwa kuipa hasara ya mabilioni Serikali ya Tanzania, wapelekwa Takukuru

Muktasari:

Baada ya Waziri wa Ardhi, William Lukuvi kuwasimamisha kazi watumishi 183 wanaodaiwa kuingilia mfumo wa ukadiriaji wa kodi ya ardhi na kusababisha upotevu mkubwa wa mapato, naibu wake, Angelina Mabula amesema wizara hiyo imepoteza mabilioni ya fedha kwa uhalifu huo

Dar es Salaam. Baada ya Waziri wa Ardhi, William Lukuvi kuwasimamisha kazi watumishi 183 wanaodaiwa kuingilia mfumo wa ukadiriaji wa kodi ya ardhi na kusababisha upotevu mkubwa wa mapato, naibu wake, Angelina Mabula amesema wizara hiyo imepoteza mabilioni ya fedha kwa uhalifu huo.

Watumishi hao ambao waziri Lukuvi ameyakabidhi majina yao kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya uchunguzi, wanadaiwa kuingilia mfumo wa kukadiria na kukusanya kodi ya pango ya ardhi kinyume na utaratibu na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

Taarifa iliyotolewa juzi jioni na ofisa habari wa wizara hiyo, Hassan Mabuye inasema kwamba Waziri Lukuvi amemwagiza katibu mkuu kuwasilisha orodha ya watumishi hao Takukuru ili uchunguzi uanze.

Waziri Lukuvi jana hakupatikana kutoa ufafanuzi wa suala hilo, lakini naibu waziri Mabula alisema Serikali imepoteza mabilioni ya fedha kwa mchezo huo.

“Zinafahamika ni bilioni za pesa zinangoja uchunguzi, siwezi kukupa kiasi kamili. Tukimaliza (uchunguzi) ndiyo tutajua ni kiasi gani. Lakini ni mabilioni ya fedha,” alisema Mabula.

Alidai kuwa uhalifu huo umefanywa na watumishi hao katika maeneo yao ya kazi na ndiyo maana uchunguzi unafanyika.

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Agosti 9, 2019