Wavaaji wa miwani ya urembo hatarini kuharibu macho yao

Monday April 22 2019
pic miwani

Tanga. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewatahadharisha wananchi juu ya uvaaji wa miwani urembo na matumizi ya dawa za macho bila ushauri wa daktari kuwa ni hatari kwa afya zao.

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa sasa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa macho nchini kutokana na kasi ya uvaaji wa miwani hiyo na matumizi ya dawa kiholela.

Waziri Ummy alisema hayo juzi alipokuwa akizindua kambi ya kutibu macho iliyoandaliwa na asasi ya maendeleo ya wanawake Mkoa wa Tanga (Tawode), kwa kushirikiana na Taasisi ya Bilal Muslim Mission ya Tanzania chini ya udhamini wa shirika la Better Charity kutoka Uingereza.

Waziri Ummy alisema takwimu za waliojitokeza kupima macho zinaonyesha kuwa kila watu 100, wanne kati yao wanakabiliwa na ubovu wa macho na idadi hiyo inaweza kuongezeka kama wananchi hawatachukua hatua za kujikinga.

Alisema kingine kinachochangia kuharibika kwa macho ni watu kula vyakula visivyo na vitamini A na kula kwa ‘mawazo’ mboga za majani na matunda.

“Kati ya hawa Watanzania 100, wanne kati yao wanasumbuliwa na ubovu wa macho na mmoja hubainika akiwa na tatizo la upofu na watatu wanasumbuliwa na uoni hafifu na wa kati,” alisema Ummy.

Advertisement

Waziri huyo alisema jicho ni kiungo muhimu cha mwili wa mwanadamu na akashauri kuwa ni vyema watu wakahudhuria kliniki za macho pale wanapoona dalili za ugonjwa.

“Ukiona una tatizo la macho nenda kwenye vituo vya afya ukafanyiwe uchunguzi ili upate matibabu ya haraka, lakini nawahimiza, hakikisheni mnachunguza afya ya macho na ya kinywa mara moja kila mwaka,” alisema Waziri Ummy.

Alisema watu 100 wanaokwenda kutibiwa maradhi hayo ya macho mapema, 80 kati yao hupona.

Mwenyekiti wa Bilal Muslim Mision Africa, Mohsin Abdallah Sheni alisema taasisi hiyo inatoa huduma kwenye maeneo wanayobaini kuwa na matatizo na mahitaji.

Alisema katika kambi hiyo ya siku nne, wanatarajia kutoa huduma kwa watu 2,000 ambao watapata vipimo na matibabu bure pamoja na kupatiwa miwani ya kusomea, kuona na ya jua.

Mwandishi wetu alishuhudia idadi kubwa ya wakazi wa Tanga na vitongoji vyake wakiwa wamejitokeza katika kambi hiyo iliyopo makao makuu ya Maawal Islamu jijini hapa wakisubiri huduma hiyo.

Advertisement