Waziri amuondoa mhandisi kusimamia mradi wa umeme wa Kinyerezi I

Muktasari:

Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme (Tanesco) kumwondoa mhandisi wa mradi wa Kinyerezi I, Hillary Towo kusimamia mradi wa umeme wa Kinyerezi I baada mkandarasi wake ambaye ni kampuni ya Jacobsen Elektro kusitisha ujenzi bila taarifa

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme (Tanesco) kumwondoa mhandisi wa mradi wa Kinyerezi I, Hillary Towo kusimamia mradi wa umeme wa Kinyerezi I baada mkandarasi wake ambaye ni kampuni ya Jacobsen Elektro kusitisha ujenzi bila taarifa.

Kalemani amechukua hatua hiyo leo Jumanne Agosti 13, 2019 alipotembelea mradi huo baada ya kupata taarifa kuwa umesimama kwa mwezi mmoja sasa na mkandarasi ameondoka nchini.

Kalemani amesema haiwezekani mradi umesimama mwezi mzima na mkandarasi ameondoka bila Serikali kuwa na taarifa wakati msimamizi wa mradi huo yupo.

Amemuagiza mkurugenzi wa Tanesco, Tito Mwinuka kuweka mhandisi mwingine wa kusimamia mradi huo.

"Nataka kazi ziendelee, huyu bwana (Towo) weka pembeni, haiwezekani mkandarasi ameondoka mwezi mzima umepita. Kwanini asitoe taarifa vyombo vya dola vitusaidie katika hili?" amehoji Waziri Kalemani.

Waziri huyo pia ameitaka Tanesco kuzuia pasi ya kusafiria ya meneja mradi wa kampuni ya Jacobsen Elekro, Markku Repo mpaka atakapokamilisha mradi huo Septemba, 2019. Amemtaka Repo kuwaita wafanyakazi wengine walioondoka kuja kumalizia kazi iliyobaki.

Awali,  akimweleza Waziri Kalemani kuhusu mradi huo, Towo amesema walipokea barua mwezi uliopita kutoka kwa mkandarasi akidai kwamba wamefilisika, hivyo hawatoweza kuendelea na kazi tena.

Alipoulizwa na Kalemani  kama alitoa taarifa, mhandisi huyo amesema aliandika barua. Hata hivyo Waziri alisisitiza kwamba hakupata taarifa hiyo.

Katika mradi huo utakaozalisha umeme wa MW 185, tayari mkandarasi amelipwa Dola 129 milioni za Marekani kati ya Dola 180 milioni anazotakiwa kulipwa kwa mradi mzima.

Mradi huo wa Kinyerezi I ulitakiwa kukamilika mwezi huu, hata hivyo Waziri Kalemani ameagiza mradi huo kukamilika mwezi ujao.