Bashiru Ally ataja sifa za wagombea uchaguzi wa Serikali za mitaa

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema atakayejihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa chama hicho tawala kusaka wagombea wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, atapoteza sifa za kugombea.

Muleba. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema atakayejihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa chama hicho tawala kusaka wagombea wake katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, atapoteza sifa za kugombea.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 30, 2018 alipokutana na wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya za Muleba na Biharamulo mkoani Kagera.

Amesema kila kiongozi wa CCM atakayejitokeza kugombea uenyekiti wa kijiji au mtaa, lazima awe mwadilifu na mwaminifu.

Amebainisha kuwa baadhi ya wagombea wanatumia majukwaa kupinga rushwa licha ya kuwa wanajihusisha nayo, ikiwa ni pamoja na kukiuka maadili ndani ya chama.

"Makatibu wa CCM kila ngazi hata nyie msiwe wa kupokea rushwa kupitisha majina ya wagombea wasiokuwa na sifa lazima kiongozi afuate miiko na ahadi za mwanachama,” amesema Bashiru.

Alitumia nafasi hiyo kuzungumzia migogoro ya ardhi, kuziagiza halmashauri za wilaya hizo na nyingine nchini Tanzania kutatua migogoro ya ardhi kati ya wananchi na taasisi mbalimbali.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Kagera Costansia Buhiye ameahidi kusimamia kanuni na sheria za chama hicho tawala kuhakikisha viongozi watakaojitokeza kuwania nafasi wanakuwa waadilifu na waaminifu.