Korti yasema Nondo ana kesi ya kujibu

Mwenyekiti Wa mtandao Wa wanafunzi  vyuo vikuu Abduli Nondo akitoka Mahakamani baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.

Muktasari:

Nondo atajitetea kwa njia ya kiapo na atakuwa na mashahidi watano

Iringa. Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, imesema mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi wa vyuo vikuu, Abdul Nondo ana kesi ya kujibu.

Hakimu Liad Chamshama akitoa uamuzi leo Agosti 27, 2018 amesema ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na Jamhuri katika kesi unaonyesha Nondo ana kesi ya kujibu.

Amesema Nondo anatakiwa kuthibitisha maelezo aliyoyatoa kwa ofisa wa polisi.

Katika kesi hiyo Nondo anashtakiwa kwa makosa mawili akidaiwa kutoa taarifa ya uongo kwa ofisa wa polisi wa kituo Mafinga akidai alitekwa na watu wasiojulikana, kosa analodaiwa kutenda Machi 7, 2018.

Pia, anashtakiwa kwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.

Hakimu Chamshama amesema Nondo ana haki ya kujitetea kwa kiapo au bila kiapo. Pia, ana uhuru wa kupeleka mashahidi.

Wakili wa utetezi, Chance Luoga amesema mteja wake atajitetea kwa kiapo na atakuwa na mashahidi watano.

Mahakama imepanga Septemba 18 na 19, 2018 kuanza kusikiliza mashahidi wa upande wa utetezi.