Kupatikana kwa ‘Mo’ Dewji, Askofu Gwajima aibuka

What you need to know:

  • Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima leo ameongoza ibada  kanisani kwake na kuzungumzia kupatikana kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amewataka waumini wa kanisa hilo kuendelea kuliombea Taifa kwa sababu Mungu anasikiliza maombi yao ikiwamo kupatikana kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye alikuwa ametekwa.

Askofu Gwajima aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa ibada iliyohudhuriwa na mamia ya waumini katika kanisa lake.

Alisema wiki iliyopita walimwombea Mo Dewji kama ambavyo wamekuwa wakiliombea Taifa na viongozi wake na kama walivyoomba wakati wa mauaji ya watu Kibiti mkoani Pwani.

"Tuendelee kuwa watiifu katika kuliombea  Taifa letu. Mungu wetu anasikia," alisema Askofu Gwajima huku waumini wake wakipiga makofi na kushangilia.

Kanisa la Ufufuo na Uzima ni miongoni mwa makanisa yaliyofanya ibada wiki iliyopita kumwombea Mo Dewji apatikane akiwa salama baada ya kutekwa na watu wasiojulikana alfajiri ya Oktoba 11 katika Hoteli ya Colloseum jijini Dar es Salaam na jana Jumamosi bilionea huyo alipatikana baada ya kutelekezwa viwanja vya Gymkana.