Breaking News

Ukweli kuhusu UTI kwa wanaume

Friday December 27 2019

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi

Kitabibu mambukizi kwa njia ya mkojo kwa wanaume, hujulikana kama Urinary Track Infections(UTI).

Huu ni uambukizaji unaohusisha mfumo wa mkojo; yaani figo, mirija inayopeleka mkojo katika kibofu, kibofu cha mkojo na mrija wa kutolea mkojo (urethral). Vijidudu vinavyochangia maambukizi ya tatizo hili huwa ni bakteria, fangasi (yeast) na mara chache sana virusi.

Mara nyingi wanaume wamekuwa wakipata hofu ya tatizo hili na baadhi wanaouliza maswali wamekuwa wakidhani kuwa lina uhusiano wa moja kwa moja na magonjwa ya zinaa.

Baadhi ya magonjwa yatokanayo na ngono zembe yanaweza kuwa dalili za kama zile za UTI, ikiwamo kuhisi maumivu au kuungua wakati wa kukojoa.

Magonjwa ya zinaa huwa na nyongeza kwa kutoa uchafu mweupe kama maziwa katika njia ya mkojo au usaha.

Tatizo la UTI ni mara chache sana kuwapata wanaume katika maisha yao, na kama ikiwapata huwa ni wanaume ambao umri umesogea yaani wazee wenye miaka 50 kuendelea. Huwapata watoto wadogo, vijana na watu wazima ambao huwa ni kwa sababu ya matatizo ya kimaumbile. Wanawake wanapata tatizo hili sana kutokana na maumbile yao ikiwamo uwapo wakaribu wa maeneo ya uke na njia ya haja kubwa. Bakteria waliopo njia hiyo ndio wanasababisha tatizo hili.

Advertisement

Bakteria hao hujulikana kama E.Coli ambao wakiwa njia ya haja kubwa hawana athari ila wanapohama eneo jingine la mwili huweza kusababisha uambukizi. Kwa kawaida wanaume hawapati sana UTI kutokana na kuwa na maumbile tofauti ikiwamo kuwa na mrija mrefu wa kutolea mkojo kuliko kina mama jambo ambalo ni faida kwao.

Wanaume walio katika hatari ya kupata UTI ni wenye miaka zaidi ya 50, wenye tatizo la kuvimba tezi dume, kisukari, mawe katika figo au kibofu na upungufu wa kinga mwilini, wasiotahiriwa na wenye kuwekewa mrija wa mkojo.

Dalili anazopata mwanamke ni sawa na zile anazopata mwanaume, waathirika wa tatizo hili au wanaodhani wana tatizo hilo hueleza dalili mbalimbali kama mkojo kuwa na harufu kali na kwenda haja mara tu baada ya kukojoa. Vile vile mkojo kuwa na rangi nyeupe/kijivu wenye kiwingu, maumivu wakati wa kukojoa, kuhisi kuungua wakati wa kukojoa, uwepo wa damu katika mkojo, maumivu ya kiuno na mgongo.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu

Advertisement