LIGI YA MABINGWA AFRIKA: Tuone sasa mavitu ya Simba SC

Monday December 31 2018

 

By Charles Abel,Mwananchi [email protected]

Droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ratiba yake ilichezeshwa jijini Kairo, Ijumaa iliyopita na wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano hayo, Simba waliangukia Kundi D.

Kwenye kundi hilo, Simba ambayo iliingia hatua hiyo kwa kuitoa Nkana Red Devils ya Zambia imepangwa sambamba na timu za Al-Ahly ya Misri, AS Vita (DR Congo) na JS Saoura ya Algeria.

Ni kundi gumu kwa Simba ukizingatia inakutana na timu za Al-Ahly na AS Vita ambazo kwenye mashindano yaliyopita ya Afrika kwa ngazi ya klabu zilifika hatua ya fainali na kupoteza lakini pia Saoura nayo inaonekana ni tishio kutokana na kitendo chake cha kuwafungisha virago Ittihad Tanger ambaoo ni bingwa wa Morocco.

Pamoja na hilo, uwepo wa timu mbili kutoka mataifa ya Kaskazini mwa Afrika yanayozungumza Kiarabu unaongeza presha kwa Simba kwani wawakilishi hao wa Tanzania rekodi zinaonyesha wamepoteza michezo yote waliyocheza ugenini dhidi ya timu za Uarabuni zaidi ya sare na ushindi kwa mikwaju ya penalti.

Kuelekea hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Spoti Mikiki inakuletea tathmini fupi ya timu za JS Saoura, Al-Ahly na AS Vita ambazo zimepangwa pamoja na Simba kwenye Kundi D.

Al-Ahly

Wakali hao wa Misri walioanzishwa mwaka 1907 na wanafunzi jijini Cairo, wanatajwa kuwa ndio klabu yenye mafanikio zaidi barani Afrika kuliko nyingine yoyote kutokana na idadi kubwa ya mataji waliyotwaa katika mashindano mbalimbali ambayo wamekuwa wakishiriki.

Al-Ahly inayotumia Uwanja wa Kimataifa wa Cairo unaoingiza mashabiki 75,000 au ule wa Al Salam wenye viti vinavyoweza kukaliwa na mashabiki 30,000 imeshinda jumla ya vikombe 132 yanayoifanya iwe klabu inayoshika nafasi ya pili kwa kutwaa mataji mengi nyuma ya Real Madrid duniani.

Timu hiyo ambayo inajulikana kwa jina la utani la ‘Mashetani Wekundu’ iko chini ya kocha raia wa Uruguay, Martin Lasarte ndio mbabe wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa wametwaa ubingwa mara nane katika miaka ya 1982, 1987, 2001, 2005, 2006, 2008, 2012 na 2013.

Imefuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa timu ya Jimma Aba ya Ethiopia kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.

AS Vita Club

Ukiachana na Al-Ahly, Simba pia itakabiliana na timu ya AS Vita Club kutoka DRC ambayo imeanzishwa mnamo mwaka 1935 na imekuwa ikikipiga Stade de Martyrs unaoingiza takribani mashabiki 80,000 ambao upo jijini Kinshasa.

Mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1973, wanaingia kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu huu wakiwa wametoka kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliomalizika ambako wamefungwa kwa jumla ya mabao 4-3 na Raja Casablanca iliyotwaa ubingwa.

Ni timu inayonolewa na kocha wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Florent Ibenge na imekuwa ikimtegemea zaidi mshambuliaji Jean Marc Makusu Mundele katika kufumania nyavu.

AS Vita ni miongoni mwa timu ambazo zina mafanikio makubwa nchini DRC ikiwa sambamba na TP Mazembe kwani imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo mara 15 na huku ikitwaa Kombe la Chama cha Soka cha huko mara tisa.

JS Saoura

Wawakilishi hao wa Algeria watakuwa wanashiriki kwa mara ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu timu hiyo ilipoanzishwa rasmi mwaka 2008 katika mji wa Meridja uliopo jimbo la Bechar nchini humo.

Jeunesse Sportive de la Saoura kwa jina la utani wanafahamika kama ‘Tai’ na wanakipiga Stade 20 Août 1955 unaoingiza mashabiki 20,000 kwa ajili ya kuchezea mechi zake za nyumbani katika mashindano mbalimbali.

Wanashika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Algeria ambayo ina jumla ya timu 16, wakiwa nyuma ya timu za USM Algers, JS Kabylie na ES Setif ambazo ni timu kongwe na maarufu nchini Algeria ambazo hata hivyo zimekosa nafasi ya kuiwakilisha nchi hiyo msimu huu.

Saoura inayoanza na Simba jijini Dar es Salaam, inaonolewa na kocha Nabil Neghiz ndio wanaanza kuibuka kwenye mashindano ya Afrika ambako wamekuwa hawana mafanikio makubwa ingawa Waalgeria wanaitazama kama mkombozi wao mpya kutokana na uwekezaji wa hali ya juu walioufanya.

Advertisement