NDANI YA BOKSI: Noma kwako tu, mwanaume kulelewa sasa ndio ‘dili’ mjini

Ebitoke

Nipo Mbezi ya chini ambako watu wanaotumia barabara ya Bagamoyo hupita kukwepa foleni ya Makongo, katika ‘supa maketi’ moja.

Nimejikuta tu nimeingia bila kupenda. Kifupi sikushirikisha ubongo na macho kujua vinataka nini kwa wakati huo. Naangazaangaza mimacho tu kama mgombea wa serikali za mitaa aliyekatwa jina na mtendaji.

Si mapenzi yangu bali ni nguvu ya ibilisi na pepo ambavyo vilimtumia binti mmoja kunivuruga akili na kujikuta namfuata kokote kule aendako. Ni kama kile kiumbe cha kijuha kwenye mbuga zetu wenyewe mnaita fisi. Kikifuatilia mkono wa mtu kwa kudhani utadondoka kiutafune kikatili. Nilikuwa hivyo siku hiyo.

Safari ilianzia mita chache kutoka hapo. Nilipomuona mrembo huyu na kuamua kumfuatilia. Yes! Alinivutia mno kiasi kwamba angekuwa mwajiriwa ATCL ingekuwa habari ya dunia. Wateja wote wa Qatar, Itihad, Emirates, Swiss Air, SA, KQ, British na Ethiopian Airlines, wangeandamana kutaka akahudumie kwao. Yule mwanamama kule bungeni ‘aliyewanyali’ wahudumu wa ATCL bila soni. Si tu angefurahia ATCL kuajiri malaika wa ajabu. Bali pia angepeleka hoja binafsi kutaka wabunge wa viti maalumu kigezo kiwe mvuto kwanza. Huyu alikuwa na mvuto wa kuwavutia hadi malaika.

Kitu rahisi zaidi kwangu ni kuukubali urembo wa demu. Nikikutana na demu mrembo nitasema huyu ni mrembo. Mrembo nitakayesema mimi kuwa huyu ni mrembo sana hata Will Smith, Jay Z, Barack Obama, James Hadley Chase, Oscar Kambona, Sir George Kahama hata Adolf Hitler angekubaliana nami. Huyu pia alikuwa mrembo sana. Zingatia neno ‘SANA’.

Sioni ni vipi Askofu Desmond Tutu, Oliver Thambo pamoja na Anwar Sadat yule Rais wa zamani wa Misri, wangekataa kumuita mrembo sana, huyu binti niliyekutana naye. Ni aina ya wale warembo ambao walifanya Wafalme wa tawala za kale wawe wapumbavu hata kudiriki kuwatuma askari wao vitani mstari wa mbele ili wafe haraka na wao warithi wake zao.

Nilijikuta naishia kulipia ‘bili’ ya mahitaji yake pale ‘supa maketi’. Naomba tuelewane hapa. Nilitumia nguvu nyingi kumshawishi ili nilipie kana kwamba ndo natongoza rasmi. Hakuwa na njaa wala uhitaji wa kusaidiwa na bwege kama mimi. Ni kiherehere na shobo zangu tu kwa imani kuwa nikilipia ni kazi yake kuelewa kuwa nimempenda. Niombewe tu kwa hili.

Fedha inakwenda kwa mwenye nazo. Hii ndiyo lugha sahihi ya kutumia kwa tukio hili, sikuwa na fedha nyingi na huenda yule mrembo alikuwa nazo zaidi yangu lakini kile kiburi cha kiume, ujasiri wa kihayawani na imani ya kizuzu yenye wendawazimu wa kimihemko ya kizinzi. Nikajikuta natoa kwa kukokotoa yote na kulipia mahitaji ya yule binti. Mimi ‘naamuaga’ tu hata sijali.

Moyo uliuma kulipia kiasi kikubwa cha fedha kwa demu nisiyemfahamu hata kwa jina, lakini nilijikuta nakenua meno nikimtazama kiumbe husika. Nikajipiga kifuani na kusema “huu ndo uanaume wa shoka. Tumia fedha upate ujasiri wa kusaka nyingi zaidi”. Nilijipa moyo kilofalofa huku nikimsindikiza kwenye gari yake. Alizidi kunivutia. Anatembea kwa kunyata kama ardhi ina miba. Hapa ndipo nilipata wasaa wa kushuhudia uumbaji wa Mwenyezi. Si Bongo Movie wala Bongofleva wa kike wa kulingana naye hata kwa mavazi yake tu. Hakustahili kuishi Bongo. Kiswahili chake kilimuumiza koo akiongea. Anastahili kuongea lugha ya Beyonce siyo ya Amber Rutty. Acha!

Wakati akihangaika kuweka mizigo ndani ya gari, ilikuwa ndiyo nafasi yangu ya kuomba namba. Ajabu hakuwa na maswali mengi kama vitoto vya Kiswahili unakuta kibovu ila ukikiomba namba kinauliza: “Unataka namba yangu ya nini?” Lakini yeye aliitoa huku akitabasamu. Ningekuwa Mo Dewji ningenunua na ‘supa maketi’ yote iwe yake milele Amina.

Hawa kina Hawa? Ni zaidi ya Twiga kwenye mbuga zetu. Hawa ndo vivutio bora zaidi katika uso wa dunia hii. Acha kabisa. Ili ujue mvuto wa viumbe hawa, mpaka mheshimiwa wa jinsia ya kike huko bungeni, naye anataka shirika la ndege ATCL, liajiri viumbe wenye mvuto kama huyu. Ina maana kuna totozi wanaomvutia zaidi na yeye kwenye mboni zake.

Kama mwanamama naye anavutiwa na kina Hawa mimi ni nani hata nisivutwe nao niwaonapo? Mengine muwe mnasamehe tu ndugu zangu si mapenzi yetu bali ni makusudi ya Mungu Baba. Kwa kutuumbia malaika wanaoishi nasi duniani. Huyu alifaa kuishi na malaika wenzake mbinguni, si hapa duniani na kina Dogo Janja.

Niliachana naye pale pale ‘supa maketi’ kwa ahadi za kuwasiliana. Ingawa sikuwa wazi nitawasiliana naye kwa ajili ya nini, lakini mwitikio wake bila shaka alielewa kuwa ni nini. Alielewa nataka kumpa kile ambacho yule Bongo Movie anakililia kwa msela wa Mbeya.

Uchumi kwa sasa unashikiliwa na kina dada hatutaki kusema ukweli, lakini kwa dhati ya moyo nasema kuwa dunia inaendeshwa na mwanamke kwa mgongo wa mwanaume. Tunakoelekea tutajikuta mwanaume ni roboti la kutengeneza miundombinu ya totozi. Ile 50 kwa 50 imevuka malengo ya kule Beijing na sasa imekuwa dhahama.

Mama Getrudi Mongela aliyesimamia ule mchongo yungali hai. Sijajua anafurahia malengo yao kupita kipimo au anaumizwa. Kuona kaka, watoto na wajukuu zake wa kiume tunavyoumia mitaani kwa kuendeshwa kama maboya na watoto wa kike? Tunaendeshwa kama magari ya taka nasi bila haya tunaona ni ufahari, fuatilia maofisini mpaka mitaani.

Tunalazimika kukopa kwa ajili ya totozi. Mnafanya kazi pamoja, kipato kinalingana kwa maana ya mshahara, lakini ukileta stori za ‘bebi bebi’ umeumia. Mshahara wako utatumika wote yeye akipeleka kwenye vikoba na kutuma kwa mama Machame huko. Mshahara wa totoz ni kwa ajili ya vikoba, saluuni na mavazi.

Mshahara wa baba ni chakula, ada kwa watoto, pango la nyumba, kusaidia ukweni, kusomesha watoto hata ndugu wa mkewe au mwanamke wake. Hata mkiachana jukumu lako kulea na kusomesha watoto wote. Usisahau pia mshahara huo huo uende kwenye vikao vya jioni baa na totozi amazing. Miaka ijayo matajiri wakubwa watakuwa kina mama.

Leo hii Ebitoke anasema kuwa anamlea Yusuf Mlela. Miaka ya nyuma hata angeongea kwa utani tu ingekuwa kashfa mbaya sana kwa mwanaume kulelewa. Leo inaonekana kama ufahari kulelewa. Mlela haonyeshi kuumizwa na hayo anaona ni haki yake kabisa kusemwa hivyo. Dunia imepinduka miguu juu kichwa chini. Tumekausha tu.

Ben Pol humsikii kwa ubora wa tungo na sauti yake kimuziki. Taarifa zake nyingi zinahusu maisha ya kifahari anayopewa na demu wa Kikenya. Labda anaona sifa na fahari kubwa kuongelewa kwa namna hiyo. Hajali na humsikii kulalamika na zaidi anajitutumua kwa kuposti picha zake za bata la demu analopewa duniani. Hii inaitwa noma kwako.

Si kwamba Ben Pol peke yake ndo anaona ufahari, hata wanaomuhoji huona raha kuuliza taarifa hizo. Wanahabari wa magazeti, radio na runinga wako ‘bize’ na malezi ya mama wa Kenya kwa kaka yao kuliko muziki wake. Habari za muziki si dili tena kwake.

Je, ni wangapi watabeba majukumu ya mwanamke? Fedha yake itakuwa inafanya nini? Hakuna.

Itarundikana na mwisho wa siku ataamua kumlea Ben Pol au Mlela wake amtakaye. Marioo wengi hulelewa kwa fedha za wanaume. Kiasili ni ngumu sana mwanamke kulea mwanaume kwa fedha za jasho lake. Walezi wengi wa marioo hufanya hivyo kwa zilizozidi kwa hongo ya wanaume. Mishahara yao inakutana na mingine. Hapo katikati kuna mishahara mtambuka toka kwa mazuzu kama sisi. Tuelewane. Siongelei kina mama wapambanaji, wale waliosoma au kufanya kazi kwa bidii. Hao huwezi kukuta wanalea vitoto vya kiume kisimbilisi. Hao huwa ‘bize’ na familia pamoja na maendeleo ya jamii yake. Hapa naongelea ndezi za kike zinazojivika ufugaji wa ng’ombe za kiume (marioo) zisizotaka kufanya kazi.

Wanaume wametoweka kama mikutano ya kisiasa. Wengi wametoboa masikio kama dada zao. Wamesuka kama mama zao. Wanarembua kama dada poa. Wamelegea kama nyaya za simu za mezani. Wanalamba midomo kama totozi watongozwapo. Wanapaka poda na kupoteza muda kwenye kioo kuliko dada zao. Kwishnei.

Tuna kila kitu na hatujafika popote zaidi ya kurukaruka kama bisi kikaangoni.