TULONGE AJIRA : Unataka kuwa mfanyabiashara au mjasiriamali mwenye mafanikio?

Friday March 1 2019Mpoki  Mwaiswaswa

Mpoki  Mwaiswaswa 

By Mpoki Mwaiswaswa

Watu wengi wanaofanya kazi serikalini, sekta binafsi au ambao hawana ajira, wanashauku ya kujiajiri.

Kila siku huwa wanasikia kutoka kwa wengine kwamba ujasiriamali au biashara inalipa.

Ni kweli ujasiriamali unalipa kama utakubali kuingia gharama za msingi katika biashara husika.

Hakuna mafanikio katika biashara au ujasiriamali pasipo kulipa gharama ya muda, pesa na maarifa.

Ikiwa unataka kuwa mfanyabiashara huna budi kutambua kuwa ujasiriamali ndiyo kazi yako na inakuhitaji wakati wote ili iweze kukua.

Hivyo, kama unapanga kujiingiza kwenye ujasiriamali ni muhimu kufahamu safari ya kufanikiwa siyo rahisi hata kidogo.

Advertisement

Safari inakuhitaji ujitoe, uwe tayari kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya watu walioajiriwa.

Pia, uwe tayari kufanya kazi nyingi zaidi ya mtu aliye kwenye ajira. Unapoanzisha biashara yako unatakiwa kuvaa kofia nyingi katika biashara kwa wakati mmoja.

Unaweza kuwa mmiliki wa biashara husika, ofisa masoko, mhasibu, ofisa mauzo na wewe ndiye mtafiti wa mambo mbalimbali kuhusu biashara yako. Hayo yote hayafanyiki pasipo kuingia gharama, lazima utafute ujuzi na ufahamu mambo sahihi katika biashara hiyo kwa gharama yoyote.

Ni muhimu kufahamu maeneo muhimu ili ujue ni wapi panahitajika kuwekeza nguvu zaidi.

Ukitaka kuwa mfanyabiashara au mjasiriamali mwenye mafanikio kibiashara ni lazima ujisukume kufanya kazi hata pale ambako hujisikii kufanya hivyo. Jambo muhimu ni kujiongeza mwenyewe kiutendaji, kiujuzi, kimaarifa, kimbinu na kimkakati katika biashara yako ili uwe na faida endelevu na imara katika soko lolote lenye ushindani.

Changamoto kubwa miongoni mwa Watanzania wanaoanza biashara au ujasiriamali hawako tayari kulipa gharama za kujiongeza kiuwezo na kimaarifa katika biashara zao ili ziwe na faida endelevu.

Wengi wapo tayari kulipa gharama kwenye mambo yasiyo na tija katika biashara zao kama vile starehe, anasa na mambo mengine yasiyo na msaada kwao.

Kama unataka kufanikiwa katika biashara au ujasiriamali usiwe unasubiri kupangiwa nini cha kufanya au kusukumwa ndiyo uweze kutekeleza majukumu yako.

Kwa elimu, ushauri na mafunzo kuhusu ujasiriamali, biashara na kilimo tembelea kurasa zetu Facebook, Twitter na Instagram kwa jina la ‘Elimika Ung’are’ au piga namba 0766656758/0655056758

Advertisement