Mahitaji ya kisheria katika usajili wa kiwanda

Kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji Leseni za Viwanda, ikisomwa pamoja na Kamusi Kuu ya Kiswahili; kiwanda ni mahali panapofanyika shughuli ya kiuchumi inayohusisha uchakataji wa malighafi na uzalishaji wa bidhaa au ni jengo lenye vifaa, mashine mbalimbali na wafanyakazi linalozalisha bidhaa au malighafi.

Sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji Leseni za Viwanda sura ya 46 ya mwaka 2002, imeweka wazi kuwa kila raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana haki ya kuanzisha na kupata leseni ya kiwanda kwa mujibu wa sheria.

Sheria hii pia inaruhusu wageni kutoka nchi mbalimbali kuja nchini kusajili na kuanzisha viwanda ili mradi tu, wawe wamefuata sheria zote zinazohusiana na usajili wa makampuni, kodi, vibali vya kazi, vibali vya ukaazi na taratibu nyingine zinazohusiana na sekta husika.

Sheria imeeleza kuwa kuna aina mbili za viwanda katika mchakato wa usajili na utoaji leseni.

Aina ya kwanza ni viwanda vidogo ambavyo mtaji wake na uwekezaji wake hauzidi Sh100 milioni. Viwanda hivi hupewa cheti cha usajili. Aina ya pili ni viwanda vikubwa ambavyo mtaji wake na uwekezaji wake unazidi Sh100 milioni na hupatiwa leseni ya kiwanda. Pamoja na vigezo vingine vinavyohitajika kisheria ili kuanzisha kiwanda, nyaraka za msingi ambazo muombaji anapaswa kuziwasilisha ni za usajili wa kampuni, cheti cha mlipa kodi, leseni ya biashara, vibali vya kisekta vya uzalishaji bidhaa husika, uthibitisho wa umiliki wa eneo la kiwanda kwa kuwasilisha mkataba wa pango ulioandaliwa kisheria na kusainiwa na wakili au hati miliki ya eneo.

Nyaraka nyingine ni ripoti ya athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza kutokana na kiwanda hicho, mpango wa biashara na fomu ya maombi ya usajili wa kiwanda.

Kwa upande wa viwanda vidogo, maombi ya usajili wa kiwanda huwasilishwa kwa msajili wa viwanda ambaye yuko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Wakala wa Usajili na Leseni (Brela). Msajili baada ya kupitia maombi hayo na kujiridhisha kuhusu uanzishwaji wa kiwanda hicho atatoa cheti cha usajili wa kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na masharti kama yako kuhusiana na uendeshaji wa kiwanda husika.

Kwa upande wa viwanda vikubwa, waombaji wanapaswa kuwasilisha maombi yao kwenye bodi ya leseni za viwanda, iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Wakala wa Usajili na Leseni (BRELA).

Bodi ya Leseni za Viwanda hukutana kila baada ya miezi mitatu kupitia maombi yaliyowasilishwa. Baada ya bodi kupitia maombi husika na yakikubalika, Msajili wa viwanda au Msajili Msaidizi kwa mujibu wa sheria, atatoa leseni ya muda mfupi kwa kiwanda hicho ambayo hudumu kwa muda wa miaka mitatu tu.

Leseni hii ya muda mfupi hutolewa ili kuwapa muda wahusika kutimiza vigezo vyote vilivyoainisha katika masharti ya utoaji wa leseni husika. Endapo masharti hayo yatakuwa yametimizwa, basi kiwanda hicho kitapatiwa usajili wa kudumu kwa mujibu wa sheria ya Taifa ya Usajili na Utoaji Leseni za Viwanda

Jambo la muhimu sana na la kuzingatia ni kufahamu kwanza nini unapaswa utimize vigezo gani ili uweze kusajili kiwanda chako na usikurupuke.

Pata muda wa kutosha wa kujifunza kwa wengine walioanisha tayari viwanda na hasa vinavyofanana na kile unachotaka kuanzisha na pata pia ushauri wa wataalamu mbalimbali wanaohusika katika uanzishwaji wa kiwanda hicho wakiwemo wanasheria ndipo uanze safari ya kudumu ya uanzishwaji na uendeshaji wa kiwanda.